Kutakuwa na kamati teule ya Baraza la Kitaifa itakayojulikana kama Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Katiba itakayowajibikia kusimamia utekelezaji wa Katiba hii, na ambayo, miongoni mwa vitu vingine–
- (a) Itapokea ripoti za kila mara kutoka kwa Tume ya Utekelezaji wa Katiba ikiwa ni pamoja na ripoti kuhusu–
- (i) Kuandaa sheria inayohitajika na Katiba hii na changamoto zozote kuihusu;
- (ii) Hatua za kuunda tume mpya;
- (iii) Hatua ya kuunda miundo misingi inayohitajika kutekeleza shughuli za kila kaunti kwa njia mwafaka pamoja na hatua za kutambua afisi na mabaraza pamoja na kuajiri na kuhamisha wafanyikazi.
- (iv) Ugatuzi wa mamlaka na majukumu kwa kaunti chini ya sheria iliyozingatiwa katika sehemu ya 15 ya Mpangilio huu; na
- (v) vizuizi vyovyote katika hatua za utekelezaji wa Katiba hii.
- (b) Kushirikiana na Mwanasheria Mkuu, Tume ya Utekelezaji wa Katiba na kamati husika za Bunge kuhakikisha sheria inayohitajiwa na Katiba hii imewasilishwa na kupitishwa kwa wakati ufaao; na
- (c) Kuchukua hatua mwafaka za ripoti ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo yoyote katika utekelezaji wa Katiba hii.