(1) Isipokuwa Mpangilio huu uonyeshe vinginevyo, mtu ambaye mara tu kabla ya tarehe ya kutekelezwa kwa Katiba hii alikuwa anahudumu au anashikilia afisi kwa muda katika afisi iliyoundwa na Katiba ya awali, kufikia tarehe ya kutekelezwa kwa Katiba hii ataendelea kuhudumu au kushikilia afisi hiyo chini ya Katiba hii kwa muda wote, iwapo kuna kipindi chochote kilichosalia, cha mtu huyo.
(2) Kwa mujibu wa ibara ndogo ya (7) na ibara ya 24, mtu ambaye mara tu kabla ya tarehe ya kutekelezwa kwa Katiba hii alikuwa na afisi au alikuwa anashikilia afisi ya umma iliyoundwa na sheria, ambayo bado inaafikiana na Katiba hii, ataendelea kuhudumu katika afisi hiyo au kuishikilia kana kwamba amefanyiwa uteuzi chini ya Katiba hii.
(3) Masharti ya sehemu hii hayataathiri mamlaka aliyopewa mtu yeyote au wajibu chini ya Katiba hii au sheria ya kuvunjilia mbali afisi au kumwondoa mtu kutoka katika afisi inayorejelewa katika ibara ndogo ya (2).
(4) Kama mtu ameondoka katika afisi ambayo alikuwa anahudumu kabla ya tarehe ya kutekelezwa kwa Katiba hii, na ofisi hiyo ipo au imeundwa chini ya Katiba hii, mtu huyo anaweza, kama amehitimu, kuteuliwa upya, kuchaguliwa, au kuteuliwa kuhudumu katika afisi hiyo kwa mujibu wa Katiba hii, isipokuwa pale ambapo Katiba hii imeonyesha kinyume.
(5) Majukumu ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma yatatekelezwa na Mwanasheria Mkuu mpaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ateuliwe chini ya Katiba hii.
(6) Majukumu ya Msimamizi wa Bajeti yatatekelezwa na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu hadi Msimamizi wa Bajeti atakapoteuliwa chini ya Katiba hii.
(7) Licha ya ibara ndogo ya (1), Mwanasheria Mkuu na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu wataendelea kuhudumu afisini kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na miwili baada ya tarehe ya kutekelezwa kwa Katiba hii, na uteuzi utakaofuata katika afisi hizi utakuwa chini ya Katiba hii.