(1) Kutabuniwa Mahakama Kuu ambayo–
- (a) inajumuisha idadi ya majaji kama itakavyobainishwa na Sheria ya Bunge; na
- (b) imeundwa na kusimamiwa kulingana na Sheria ya Bunge.
(2) Kutakuwa na Jaji Kinara wa Mahakama Kuu ambaye atachaguliwa na majaji wa mahakama ya Juu kutoka miongoni mwao.
(3) Kulingana na ibara ya (5), Mahakama Kuu ina–
- (a) mamlaka asilia yasiyokuwa na mpaka katika masuala ya uhalifu na masuala ya kiraia;
- (b) mamlaka ya kubaini iwapo haki au uhuru wa kimsingi katika Sheria ya Haki imenyimwa, kukiukwa, kuingiliwa au kutishiwa; au
- (c) mamlaka ya kusikiliza rufaa ya uamuzi wa mahakama maalum iliyoteuliwa chini ya Katiba hii kuchunguza kuondolewa kwa mtu kutoka afisini, tofauti na Tume iliyoteuliwa chini ya Kifungu cha 144;
- (d) mamlaka ya kusikiliza swala lolote kuhusu kufasiriwa kwa Katiba hii pamoja na kutoa uamuzi wa–
- (i) swali iwapo sheria yoyote inakiuka au kwenda kinyume na Katiba hii;
- (ii) swali iwapo chochote kinachosemwa kutekelezwa chini ya mamlaka ya Katiba hii au sheria yoyote, kinakiuka au kutekelezwa kinyume na Katiba hii;
- (iii) suala lolote linalohusu mamlaka ya kikatiba ya taasisi za serikali kwa mujibu wa serikali za kaunti na suala linalohusu uhusiano wa kikatiba kati ya viwango vya serikali; na
- (iv) swali linalohusu mkinzano wa sheria chini ya Kifungu cha 191.
(4) Suala lolote linalothibitishwa na mahakama kuwa linazua utata mkubwa kisheria chini ya ibara ya (3) (b) au (d) litatasikilizwa na idadi isiyo shufwa ya majaji, wasiopungua watatu , watakaoteuliwa na Jaji Mkuu.
(5) Mahakama Kuu haina mamlaka kuhusiana na masuala–
- (a) yaliyotengewa mamlaka ya kipekee ya Mahakama ya Juu chini ya Katiba hii; au
- (b) yaliyo chini ya mamlaka ya mahakama yaliyotajwa katika Kifungu cha 162(2).
(6) Mahakama Kuu ina mamlaka ya kusimamia mahakama ndogo na mtu yeyote, asasi au halmashauri, inayotekeleza jukumu la kimahakama au jukumu la mahakama ya kubuni, lakini siyo mahakama ya juu.
(7) Kwa malengo ya ibara ya (6), Mahakama Kuu inaweza kuitisha rekodi za kesi yoyote iliyoko katika mahakama ndogo, au mtu, asasi au halmashauri kama ambavyo imetajwa katika ibara ya (6) na inaweza kutoa maagizo yoyote na kutoa maelekezo inayochukulia kuwa yanafaa ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka.