(1) Rais atateua–
- (a) Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu kulingana na mapendekezo ya Tume ya Huduma ya Mahakama na kwa idhini ya Bunge; na
- (b) majaji wengine wote, kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya Huduma za Mahakama.
(2) Majaji wa mahakama za mamlaka ya juu watateuliwa kutoka miongoni mwa watu ambao–
- (a) wana shahada katika taaluma ya sheria kutoka chuo kinachotambulika, au ni mawakili wa Mahakama Kuu, au wana hitimu sawa na hizo katika masuala ya kawaida ya kisheria;
- (b) wana tajriba inayohitajika ambayo wameipata nchini Kenya na taasisi nyingine za mataifa yanayotumia mamlaka ya sheria ya Jumuia ya Madola kama zinazotajwa katika ibara ya (3) hadi (6); na
- (c) wana mienendo na maadili mema na hawabagui.
(3) Jaji Mkuu na majaji wa Mahakama ya Juu watateuliwa kutoka miongoni mwa watu ambao wana–
- (a) tajriba ya miaka kumi na mitano kama jaji katika mahakama ya mamlaka ya juu; au
- (b) tajriba ya miaka isiyopungua kumi na mitano kama msomi anayeheshimika, afisa katika idara ya mahakama, uanasheria au tajriba kama hiyo katika maeneo mengine ya taaluma ya uanasheria; au
- (c) amehitimu kwa viwango vilivyotajwa katika aya (a) na (b) kwa jumla ya miaka kumi na mitano.
(4) Kila jaji wa Mahakama ya Rufaa atateuliwa kutoka miongoni mwa watu ambao wana–
- (a) tajriba ya miaka isiyopungua kumi kama jaji wa Mahakama ya kiwango cha juu; au
- (b) tajriba ya miaka isiyopungua kumi kama msomi anayeheshimika au mwanasheria au tajriba kama hiyo katika nyanja nyingine husika ya kisheria; au
- (c) amehitimu kwa viwango vilivyotajwa katika aya (a) na (b) kwa muda wa jumla ya miaka kumi.
(5) Kila jaji wa Mahakama Kuu atateuliwa kutoka miongoni mwa watu walio na–
- (a) tajriba isiyopungua miaka kumi kama jaji katika mahakama ya kiwango cha juu; au
- (b) tajriba ya miaka isiyopungua kumi kama msomi anayeheshimika au mwanasheria au tajriba kama hiyo katika nyanja nyingine husika ya kisheria; au
- (c) amehitimu kwa viwango vilivyotajwa katika aya (a) na (b) kwa jumla ya muda wa miaka kumi.