Ruka hadi Yaliyomo

(1) Jaji wa mahakama yenye mamlaka ya juu anaweza kuondolewa tu kutoka afisini kwa misingi ya–

  • (a) kushindwa kutekeleza majukumu ya afisi kwa sababu ya ukosefu wa uwezo wa kimwili au kiakili;
  • (b) kukiuka kanuni za utendakazi zilizowekewa majaji wa Mahakama Makuu kupitia Sheria ya Bunge.
  • (c) kufilisika;
  • (d) kutokuwa na umilisi; au
  • (e) utovu wa nidhamu, ama katika utekelezaji wa majukumu ya jaji au vinginevyo.

(2) Hatua ya kumuondoa jaji kwenye wadhifa wake inaweza kuanzishwa na Tume ya Huduma za Mahakama itakayochukua hatua hiyo kivyake au kwa sababu ya malalamiko yatakayowasilishwa na mtu yeyote kwa Tume hii.

(3) Malalamiko ya mtu kwa Tume ya Huduma za Mahakama chini ya Ibara ya (2) yatawasilishwa kwa maandishi, yakionyesha ushahidi wa misingi ya madai ya kumuondoa jaji.

(4) Tume ya Huduma za Mahakama itaangalia malalamiko hayo na iwapo itaridhika kwamba ushahidi unaobainika wazi chini ya Ibara ya (1), na itatuma malamamiko hayo kwa Rais.

(5) Katika muda wa siku kumi na nne baada ya kupokea malalamiko hayo, Rais wa Taifa atamsimamisha kazi jaji huyo, na kwa kuzingatia ushauri wa Tume ya Huduma za Mahakama–

  • (a) iwapo itakuwa ni Jaji Mkuu, itateua mahakama maalum itakayowahusisha–
    • (i) Spika wa Baraza la Kitaifa kama mwenyekiti;
    • (ii) majaji watatu wa Mahakama ya Juu kutoka kwa mahakama zenye kutumia sheria ya kawaida;
    • (iii) wakili mmoja mwenye tajriba ya kazi ya miaka kumi na mitano;
    • (iv) watu wengine wawili wenye tajriba kuhusu masuala ya umma; au
  • (b) iwapo ni jaji mwingine asiye Jaji Mkuu, atateua mahakama maalum itakayohusisha–
    • (i) mwenyekiti na wanachama wengine watatu ambao wanahudumu au wamewahi kuhudumu kama jaji wa mahakama za mamlaka ya juu, au ambao wamehitimu kuteuliwa kuhudumu kwenye wadhifa huo, lakini katika kila moja ya hali hizo hawajakuwa, katika miaka mitatu inayotangulia, wamekuwa wanachama wa Tume ya Huduma ya Mahakama;
    • (ii) wakili mmoja mwenye tajriba ya kazi ya miaka kumi na mitano;
    • (iii) watu wengine wawili wenye tajriba kuhusu masuala ya umma.

(6) Licha ya Kifungu cha (160) (4), mshahara na marupurupu ya jaji ambaye anasimamishwa kazi chini ya Ibara ya (5) utapunguzwa kwa nusu hadi wakati ambapo jaji huyo ataondolewa au kurudishwa kazini.

(7) Mahakama maalum inayobuniwa chini ya Ibara ya (5)–

  • (a) itatoa kanuni za kuongoza vikao vyake kwa mujibu wa sheria inayorejelewa katika Ibara ya (10); na
  • (b) kuchunguza suala hilo kwa haraka, kutoa ripoti ya matokeo na kuwasilisha mapendekezo ya kutiliwa maanani kwa Rais.

(8) Jaji ambaye haridhiki na uamuzi wa mahakama maalum chini ya kifungu hiki, anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu kwa Mahakama ya Juu, rufaa hii itakatwa kati ya siku kumi baada mahakama maalum kutoa mapendekezo yake.

(9) Rais atatoa maamuzi kwa mujibu wa mapendekezo yaliyotolewa na mahakama maalum kufikia mwisho wa–

  • (a) kuisha kwa muda uliotolewa wa kukata rufaa chini ya Ibara ya (8), iwapo rufaa kama hiyo haikukatwa; au
  • (b) baada ya kukamilika kwa hatua zote za kesi ya rufaa chini ya Ibara ya (8), iwapo rufaa kama hiyo imekatwa na uamuzi wa mwisho unaafikiana na mapendekezo ya mahakama hiyo maalum.

(10) Bunge litatunga sheria ya kutoa kanuni za kufuatwa na mahakama maalum itakayoteuliwa chini ya kifungu cha hiki.

Msimbo wa QR unaounganisha kwenye https://blog.afro.co.ke/sw/katiba/sura-10/sehemu-2/kifungu-168/kuondolewa-afisini/