(1) Mamlaka kuu ya kaunti yamepewa, na yatatekelezwa, na kamati za mamlaka kuu za Kaunti.
(2) Kamati ya mamlaka kuu ya Kaunti inajumuisha–
- (a) gavana wa kaunti na naibu wake; na
- (b) wanachama walioteuliwa na gavana wa kaunti, kwa idhini ya baraza, kutoka kwa watu wasio wanachama wa baraza.
(3) Idadi ya wanachama walioteuliwa kwa mujibu wa ibara ya (2)(b) haitazidi–
- (a) thuluthi moja ya wanachama wa bunge la kaunti kama bunge hilo halina zaidi ya wanachama zaidi ya thelathini; au
- (b) kumi; kama baraza lina wanachama thelathini au zaidi.
(4) gavana wa kaunti na naibu wake, watakuwa afisa mkuu na naibu wa afisa mkuu wa kaunti, mtawalia.
(5) Gavana wa kaunti asipokuwepo, naibu wake ana mamlaka ya kutosha ya kuendesha shughuli zote na majukumu ya gavana wa kaunti.
(6) Wanachama wa kamati kuu ya kaunti wanawajibikia gavana wa kaunti katika utekelezaji wa majukumu na mamlaka yao.
(7) Iwapo afisi ya gavana itakuwa wazi, wanachama wa mamlaka kuu ya kaunti walioteuliwa chini ya ibara ya (2) (b) watakuwa hawana kazi.