(1) Gavana wa kaunti atachaguliwa moja kwa moja na wapiga kura waliosajiliwa katika kaunti hiyo, siku ile ya uchaguzi mkuu wa wabunge, itakayokuwa Jumanne ya pili ya mwezi Agosti, baada ya kila miaka mitano.
(2) Kuhitimu kuchaguliwa kuwa gavana wa kaunti, mtu lazima awe amehitimu kuchaguliwa kuwa mwanachama katika baraza la kaunti.
(3) Ikiwa mgombea kiti cha gavana mmoja tu atateuliwa, mtu huyu atatangazwa kuwa amechaguliwa.
(4) Ikiwa wagombea kiti cha gavana wawili au zaidi watateuliwa, kura zitapigwa katika kaunti hiyo na mgombeaji atakayepata kura nyingi zaidi atatangazwa kuwa mshindi.
(5) Kila mgombea kiti cha gavana wa kaunti atamteua mtu mmoja ambaye amehitimu kuchaguliwa kama gavana wa kaunti kuwa mgombea kiti cha naibu gavana.
(6) Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka haitaendesha uchaguzi tofauti kwa naibu gavana lakini itamtangaza mgombea aliyependekezwa na mtu ambaye amechaguliwa kuwa gavana wa kaunti kuwa amechaguliwa kama naibu gavana.
(7) Mtu hatahudumu afisini–
- (a) kama gavana wa kaunti kwa vipindi zaidi ya viwili; au
- (b) kama naibu gavana kwa vipindi zaidi ya viwili.
(8) Kwa mujibu wa ibara ya (7), mtu ambaye hajaingia afisi ya gavana wa kaunti atachukuliwa kuwa amehudumu kwa kipindi kizima, kwa mujibu wa kifungu cha 182 (3) (b).