(1) Bunge litatunga sheria ili kuhakikisha kwamba serikali za kaunti zimepokea usaidizi wa kutosha kuziwezesha kutekeleza majukumu yao.
(2) Serikali za kaunti zitaendesha mifumo ya usimamizi wa fedha inayoafikana na matakwa ya sheria ya kitaifa.
(3) Bunge litatunga sheria itakayoruhusu serikali ya kitaifa kuingilia serikali ya kaunti iwapo–
- (a) imeshindwa kutekeleza majukumu yake; au
- (b) haiendeshi mfumo wa usimamizi wa fedha unaoambatana na matakwa ya sheria ya kitaifa.
(4) Sheria inayotawa katika Ibara ya (3) inaweza, hasa, kuipa mamlaka serikali ya kitaifa–
- (a) kuchukua hatua mwafaka ili kuhakikisha kuwa majukumu ya serikali ya kaunti yanatekelezwa na mfumo wa usimamizi wa fedha unaendeshwa inavyostahili; na
- (b) kama pana haja, ichukue jukumu la kutekeleza majukumu hayo.
(5) Sheria inayotajwa katika Ibara ya (3)–
- (a) itahitaji notisi kutolewa kwa serikali ya kaunti kuhusu hatua zozote serikali ya kitaifa inadhamiria kuchukua;
- (b) itaruhusu serikali ya kitaifa kuchukua hatua zilizo muhimu pekee;
- (c) itahitaji serikali ya kitaifa, wakati inaingilia kati, ichukue hatua ambazo zitaisaidia serikali ya kaunti kurejelea kikamilifu utekelezaji wa majukumu yake; na
- (d) kutoa utaratibu utakaowezesha seneti kuhusika vyema ili kumaliza au kutoa suluhu kwa matatizo hayo.