Ruka hadi Yaliyomo

(1) Vigezo vifuatavyo vitatumiwa kutoa uamuzi kuhusu mgao sawa uliotajwa katika kifungu cha 202 na katika sheria zote za kitaifa kuhusu serikali za kaunti kama zilivyotungwa kwa mujibu wa masharti ya sura hii–

  • (a) masilahi ya kitaifa;
  • (b) kifungu kingine ambacho kinahitajika kwa mujibu wa deni la umma na mahitaji mengine ya kitaifa;
  • (c) mahitaji ya serikali ya kitaifa yatakayoamuliwa kwa misingi ya kigezo cha kutopendelea;
  • (d) haja ya kuhakikisha kuwa serikali za kaunti zina uwezo wa kutekeleza majukumu zilizopewa;
  • (e) uwezo wa kifedha na ufanisi wa serikali za kaunti;
  • (f) maendeleo na mahitaji mengine ya serikali za kaunti;
  • (g) tofauti za kiuchumi miongoni na kati ya kaunti na sababu ya kutatua matatizo hayo;
  • (h) haja ya kuchukua hatua kwa mujibu wa maeneo na makundi yaliyotengwa;
  • (i) haja ya kuboresha uchumi kwenye kila kaunti na kutoa motisha kwa kila kaunti kuboresha uwezo wake wa kuzalisha mapato;
  • (j) kutamani mgao wa mapato ulio thabiti na unaoweza kutabirika; na
  • (k) haja ya wepesi katika kukabiliana na majanga na mahitaji mengine ya muda katika misingi ya kigezo cha kutopendelea.

(2) Kwa kila mwaka wa fedha, mgao unaolingana wa mapato yanayozalishwa na taifa ambayo yatagawiwa serikali za kaunti hayatapungua asilimia kumi na tano ya mapato yote ambayo serikali ya kitaifa inayozalisha.

(3) Jumla ya fedha zilizotajwa katika Ibara ya (2) zitapigwa hesabu katika misingi ya ukaguzi wa juzi zaidi wa hesabu ya mapato yaliyokusanywa, kama itakavyoidhinishwa na Baraza la Kitaifa.

Msimbo wa QR unaounganisha kwenye https://blog.afro.co.ke/sw/katiba/sura-12/sehemu-1/kifungu-203/ugavi-sawa-na-sheria-za-kifedha/