(1) Kwa kipindi kisichopungua miezi miwili kabla ya kukamilika kwa kila mwaka wa kifedha, waziri anayehusika na fedha, atawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka ufuatao wa fedha kwa Baraza la Kitaifa.
(2) Makadirio yaliyotajwa katika ibara ya (1)–
- (a) yatajumlisha makadirio ya matumizi kutoka kwa Hazina ya Usawazishaji; na
- (b) itakayokuwa kwa muundo, na kwa mujibu wa utaratibu ufaao na kuambatana na kanuni zilizoratibiwa na Sheria ya Bunge.
(3) Baraza la Kitaifa litazingatia makadirio yaliyowasilishwa chini ya kifungu cha (1) pamoja na makadirio yanayowasilishwa na Tume ya Huduma za Bunge na Msajili Mkuu wa Mahakama chini ya Kifungu cha 127 na 173, mtawalia.
(4) Kabla ya Baraza la Kitaifa kuzingatia makadirio ya mapato na matumizi, kamati ya Bunge itajadili na kuchunguza makadirio hayo na kutoa mapendekezo yake kwa Bunge.
(5) Katika kujadili na kuchunguza makadirio hayo, kamati itahusisha umma na mapendekezo yake yatatiliwa maanani wakati kamati hiyo itakapowasilisha mapendekezo hayo kwa Baraza la Kitaifa.
(6) Wakati makadirio ya matumizi ya serikali ya kitaifa, makadirio ya matumizi ya mahakama na Baraza la Kitaifa, yatakuwa yameidhinishwa na Baraza la Kitaifa, yatajumlishwa katika Mswada wa Matumizi ya Fedha, utakaowasilishwa kwa Baraza la Kitaifa ili kuidhinisha kutolewa kwa fedha za matumizi kutoka kwa Mfuko wa Jumla, na matumizi ya fedha hizo kwa madhumuni yaliyotajwa katika mswada.
(7) Mswada wa matumizi ya fedha uliotajwa katika ibara ya (6) hautajumlisha matumizi yanayodaiwa kutoka kwa Mfuko wa Jumla na Katiba hii au Sheria ya Bunge.