(1) Tume ya Mishahara na Marupurupu imeundwa.
(2) Tume ya Mishahara na Marupurupu inajumlisha watu wafuatao walioteuliwa na Rais–
- (a) Mwenyekiti;
- (b) Watu walioteuliwa na mashirika yafutayo, ambayo watu ambao si wanachama au waajiriwa wa mashirika hayo wameteuliwa–
- (i) Tume ya Huduma za Bunge;
- (ii) Tume ya Huduma za Umma;
- (iii) Tume ya Huduma za Mahakama;
- (iv) Tume ya Kuwaajiri Walimu;
- (v) Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi;
- (vi) Baraza la Ulinzi; na
- (vii) Seneti, kwa niaba ya serikali za kaunti;
- (c) Watu walioteuliwa, kila mmoja na–
- (i) Shirika kuu linalowakilisha vyama vya wafanyakazi;
- (ii) Shirika linalowakilisha waajiri; na
- (iii) Jopo la Muungano linaloshirikisha makundi ya wataalamu yaliyokubaliwa kisheria.
- (d) Watu walioteuliwa, kila mmoja na–
- (i) waziri anayesimamia fedha;
- (ii) Mwanasheria Mkuu; na
- (e) Mtu aliye na tajriba katika usimamizi wa wafanyakazi katika huduma ya umma, aliyeteuliwa na katibu wa Waziri anayesimamia huduma ya umma.
(3) Makamishna waliotajwa katika ibara ya (1) (d) na (e) hawatakuwa na uwezo wa kupiga kura.
(4) Mamlaka na majukumu ya Tume ya Mishahara na Marupurupu ni–
- (a) Kuweka viwango na kudhibiti mishahara na marupurupu ya maafisa wote wa serikali; na
- (b) Kushauri serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kuhusu mishahara na marupurupu ya maafisa wote wa serikali.
(5) Katika kutekeleza majukumu yake, Tume hii itazingatia kanuni zifuatazo–
- (a) Haja ya kuhakikisha kuwa mswada wa fidia wa umma unakuwa ni endelevu.
- (b) Haja ya kuhakikisha kuwa huduma ya umma ina uwezo wa kuvutia na kuweka wahudumu walio na ujuzi wanaohitajika kutekeleza majukumu yao.
- (c) Haja ya kutambua uzalishaji na utendakazi; na
- (d) Uwazi na haki.