(1) Majukumu na mamlaka ya Tume ni kama yalivyofafanuliwa katika kifungu hiki.
(2) Tume–
- (a) kwa mujibu wa Katiba hii na sheria–
- (i) itaunda na kuvunja afisi katika huduma za umma;
- (ii) itateua watu kuhudumu au kushikilia afisi pamoja na kuthibitisha uteuzi huo.
- (b) itadumisha nidhamu na kuwaondoa kazini maafisa walio katika afisi hizo au wanaozishikilia kwa muda;
- (c) itakuza maadili na kanuni zilizotajwa katika Vifungu vya 10 na 232 kote katika utoaji wa huduma za umma;
- (d) itachunguza, kufuatilia, na kutathmini usimamizi na mienendo ya wafanyakazi katika utoaji wa huduma za umma;
- (e) itahakikisha utendakazi bora katika huduma za umma;
- (f) itakuza uajiri katika huduma za umma;
- (g) itachunguza na kutoa mapendekezo kwa serikali ya kitaifa kuhusu hali za utendakazi, kanuni za utendakazi, na ustahili wa maafisa wanaotoa huduma za umma;
- (h) itatathmini na kuripoti kwa Rais na Bunge kuhusu kiwango ambacho maadili na kanuni zilizotajwa katika Vifungu vya 10 na 232 zinazingatiwa katika huduma za umma;
- (i) itasikiza na kuamua rufani kuhusu masuala yanayohusiana na huduma za umma katika serikali za kaunti;
- (j) itatekeleza majukumu na mamlaka mengine yoyote kama ilivyopewa na sheria ya nchi.
(3) ibara ya (1) na (2) hazitatekelezwa katika afisi zozote zifuatazo za huduma za umma–
- (a) afisi za Serikali;
- (b) afisi ya Balozi wa nchi za Jumuia ya madola, balozi au mwakilishi yeyote katika afisi za kibalozi za Jamhuri;
- (c) afisi au wadhifa kwa mujibu wa–
- (i) Tume ya Huduma za Bunge;
- (ii) Tume ya Huduma za Mahakama;
- (iii) Tume ya kuwaajiri walimu; au
- (iv) Tume ya Huduma za Polisi ya Kitaifa; au
- (d) afisi inayohudumia serikali ya kaunti, isipokuwa ilivyofafanuliwa katika ibara ya (2) (i).
(4) Chini ya ibara ya (2), Tume haitamteua mtu kuchukua wadhifa au kushikilia afisi kama mfanyikazi katika afisi ya Rais au ya Rais mstaafu mpaka pawe na kibali kutoka kwa Rais au Rais mstaafu.
(5) Kupitia kwa maandishi, Tume inaweza, kwa masharti au bila ya masharti, kukabidhi majukumu na mamlaka yake yoyote chini ya Kifungu hiki kwa yeyote kati ya wanachama wake, au kwa afisa yeyote, bodi au idara katika huduma za umma.