(1) Usalama wa Kitaifa ni ulinzi kutokana na vitisho vya ndani na nje ya mipaka ya Kenya, watu wake, haki zao, uhuru, mali, amani, uthabiti na maendeleo na maslahi mengine ya kitaifa.
(2) Usalama wa kitaifa wa Kenya utaimarishwa na kuhakikishwa kwa mujibu wa kanuni zifuatazo–
- (a) usalama wa kitaifa unaongozwa na mamlaka ya Katiba hii na Bunge;
- (b) usalama wa kitaifa utatekelezwa kulingana na sheria, na kwa heshima ya utawala wa sheria, demokrasia, haki za binadamu na uhuru wa kimsingi;
- (c) katika kutekeleza majukumu na mamlaka yao, idara za usalama wa kitaifa zitaheshimu uanuwai wa kitamaduni wa jamii nchini Kenya; na
- (d) uajiri katika idara za usalama wa kitaifa utabainisha uanuwai wa watu wa Kenya katika viwango sawa.