(1) Idara za usalama wa kitaifa ni–
- (a) Vikosi vya Ulinzi wa Kenya;
- (b) Huduma za Upelelezi za kitaifa; na
- (c) Huduma za Polisi za kitaifa.
(2) Lengo la kimsingi la idara za usalama wa kitaifa na utaratibu wa usalama ni kuendeleza na kuhakikisha kuwepo kwa usalama wa kitaifa kwa mujibu wa kanuni zilizotajwa katika Kifungu cha 238(2).
(3) Katika kutekeleza majukumu na mamlaka yao, idara za usalama wa kitaifa na kila mwanachama wa idara hizo hataruhusiwa–
- (a) kuwa na upendeleo kwa njia yoyote,
- (b) kuendeleza maslahi ya chama chochote cha kisiasa wala sera zake; au
- (c) kuhujumu maslahi ya kisiasa au sera zake za kisiasa ambazo ni halali chini ya Katiba hii.
(4) Mtu hataruhusiwa kubuni kikosi cha kijeshi au kikosi chenye hadhi ya kijeshi au shirika linalodai kuendeleza na kuhakikisha usalama wa kitaifa isipokuwa inavyoruhusiwa na Katiba hii au Sheria ya Bunge.
(5) Idara za uslama wa kitaifa zitakuwa chini ya mamlaka ya raia.
(6) Bunge litatunga sheria kushughulikia majukumu, utaratibu na usimamizi wa idara za usalama wa kitaifa.