(1) Baraza la Usalama wa kitaifa limeundwa.
(2) Baraza hili linahusisha–
- (a) Rais;
- (b) Naibu wa Rais;
- (c) Waziri anayehusika na ulinzi;
- (d) Waziri anayehusika na mashauri ya kigeni;
- (e) Waziri anayehusika na usalama wa taifa;
- (f) Mwanasheria Mkuu
- (g) Mkuu wa Majeshi ya Kenya;
- (h) Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za kitaifa za Upelelezi; na
- (i) Inspekta-Mkuu wa Huduma za Polisi za kitaifa.
(3) Baraza litakuwa na mamlaka ya kusimamia idara za usalama wa kitaifa na kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa sheria ya nchi.
(4) Rais atakuwa mwenyekiti wa mikutano ya baraza.
(5) Baraza litateua katibu wake.
(6) Baraza–
- (a) litaunganisha sera za humu nchini, za kigeni na za kijeshi zinazohusiana na usalama wa kitaifa ili kuziwezesha idara za usalama wa kitaifa kushirikiana na kufanya kazi kikamilifu; na
- (b) litatathmini na kukadiria malengo, kujitolea katika utendakazi, na hatari zozote kwa Jamhuri kuhusiana na uwezo wa usalama wa kitaifa.
(7) Baraza litatoa ripoti kwa Bunge kila mwaka kuhusiana na hali ya usalama nchini Kenya.
(8) Kupitia kwa idhini ya Bunge, Baraza linaweza–
- (a) kupeleka wanajeshi wa kitaifa nje ya Kenya kwa ajili ya–
- (i) kuhifadhi amani katika eneo hili au kudumisha usalama wa Kimataifa; au
- (ii) shughuli nyingine za kudumisha amani; na
- (b) kuidhinisha kupelekwa kwa majeshi ya kigeni nchini Kenya.