(1) Majeshi ya Ulinzi wa Kenya yameundwa.
(2) Majeshi ya ulinzi yanahusisha–
- (a) Jeshi la Kenya la Nchi Kavu;
- (b) Jeshi la Kenya la Wanahewa; na
- (c) Jeshi la Kenya la Wanamaji.
(3) Majeshi ya Ulinzi–
- (a) yana wajibu wa kulinda na kutetea mamlaka na mipaka ya Jamhuri;
- (b) yatasaidia na kushirikiana na idara zingine katika hali za dharuraau majanga, na kutoa ripoti kwa Baraza Kuu la Kitaifa wakati wowote yanapotekeleza shughuli kama hizo; na
- (c) yanaweza kupelekwa ili kurejesha amani katika sehemu yoyote ya Kenya inayokumbwa na machafuko, lakini kwa idhini ya Baraza Kuu la Kitaifa pekee.
(4) Uongozi katika Majeshi ya Ulinzi utabainisha tofauti za kimaeneo na za kijamii za watu wa Kenya.
(5) Baraza la Ulinzi limeundwa.
(6) Baraza linahusisha–
- (a) Waziri anayehusika na ulinzi ambaye ni mwenyekiti;
- (b)Mkuu wa majeshi ya Ulinzi ya Kenya;
- (c) Makamanda watatu wa Majeshi ya Ulinzi; na
- (d) Katibu Mkuu katika wizara inayohusika na ulinzi.
(7) Baraza–
- (a) linahusika na sera kwa ujumla, kudhibiti na kusimamia Majeshi ya Ulinzi ya Kenya; na
- (b) kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa sheria ya nchi.