(1) Kila Tume itakuwa na angalau wanachama watatu, lakini wasiozidi tisa.
(2) Mwenyekiti na kila mwanachama wa tume, pamoja na anayeshikilia wadhifa wa afisi huru–
- (a) watatambuliwa na kupendekezwa kwa uteuzi kwa namna ilivyoagizwa na Sheria ya nchi;
- (b) wataidhinishwa na Baraza Kuu la Kitaifa; na
- (c) watateuliwa na Rais.
(3) Ili kuteuliwa, mtu anastahili kutimiza vigezo vilivyowekwa na Katiba hii au Sheria ya nchi.
(4) Uteuzi wa maafisa wa tume na afisi huru utatilia maanani maadili ya kitaifa yanayorejelewa katika kifungu cha 10, na kanuni ya kwamba maafisa katika tume na afisi huru , kwa jumla, watawakilisha maeneo na jamii mbalimbali za watu wa Kenya.
(5) Mwanachama wa tume anaweza kuhudumu kwa muda.
(6) Mwanachama wa tume, au anayeshikilia wadhifa wa afisi huru–
- (a) Isipokuwa ni kutokana na cheo chake, atateuliwa kwa kipindi kimoja cha miaka sita na hatateul;iwa tena; na
- (b) Isipokuwa ni kutokana na cheo chake au anahudumu kwa muda, hataruhusiwa kutumikia afisi nyingine au kuajiriwa ili apate faida, iwe ni kazi ya serikali au ya kibinafsi.
(7) Faida au zawadi inayolipwa kwa, au kutokana na mtu kuwa mwanachama wa tume au anayeshikilia wadhifa wa afisi huru itatoka katika Mfuko wa Jumla.
(8) Faida au zawadi inayolipwa kwa, au kutokana na mtu kuwa mwanachama wa tume au anayeshikilia wadhifa wa afisi huru haitabadilishwa kwa hasara ya mtu huyo wakati anapokuwa kazini.
(9) Mwanachama wa tume au anayeshikilia wadhifa wa afisi huru hatawajibika kisheria kwa jambo lolote linalofanywa kwa nia njema katika kutekeleza kazi ya afisi hiyo.
(10) Wanachama wa tume watamchagua naibu-mwenyekiti kutoka miongoni mwao–
- (a) katika kikao cha kwanza cha Tume; na
- (b) kila inapohitajika kujaza nafasi hiyo katika afisi ya naibu-mwenyekiti
(11) Mwenyekiti na naibu-mwenyekiti hawatakuwa wa jinsia moja.
(12) Kutakuwepo na katibu wa kila tume ambaye–
- (a) atateuliwa na tume; na
- (b) atakuwa afisa mkuu wa tume.