(1) Mwanachama wa Tume (isipokuwa aliye mwanachama kutokana na wadhifa wake), au anayeshikilia wadhifa wa afisi huru, anaweza kuondolewa afisini kwa sababu ya–
- (a) ukiukaji uliokithiri wa Katiba hii au sheria yoyote ikiwa ni pamoja na kuvunja sheria katika sura ya sita;
- (b) utovu wa nidhamu ama ni katika utendakazi wa mwanachama au yule anayeshikilia wadhifa wa afisi huru;
- (c ) kutokuwa na uwezo wa kimwili au kiakili katika kutekeleza majukumu ya kiafisi;
- (d) kushindwa kufanya kazi; au
- (e) kufilisika.
(2) Mtu anayeazimia kuondolewa kwa mwanachama wa tume au anayeshikilia wadhifa wa afisi huru kwa misingi yoyote iliyotajwa katika ibara ya (1) anaweza kuwasilisha malalamiko kwa Baraza la Bunge huku akifafanua yale yote yanayothibitisha azma hiyo.
(3) Baraza la Bunge litachunguza malalamiko hayo na , iwapo litaridhika kwamba yana mashiko chini ya ibara ya (1), litatuma malalamiko hayo kwa Rais.
(4) Pindi tu baada ya kupokea malalamiko hayo chini ya ibara ya (3),Rais-
- (a) anaweza kumsimamisha kazi mwanachama wa tume au anayeshikiia wadhifa wa afisi huru huku akisubiri matokeo ya uchunguzi wa malalamiko hayo; na
- (b) atateua mahakama maalum kulingana na ibara ya (5).
(5) Mahakama hii maalum itahusisha–
- (a) mtu ambaye anahudumu, au amewahi kuhudumu kama jaji wa mahakama yenye mamlaka makuu, ambaye pia atakuwa mwenyekiti;
- (b) angalau watu wawili ambao wanastahili kuteuliwa kama majaji wa Mahakama ya Juu; na
- (c) mwanachama mwingine mmoja ambaye ana uwezo wa kuchunguza ushahidi kuhusiana na msingi mahususi wa kumtaka afisa huyo aondolewe.
(6) Mahakama maluum itachunguza suala hilo kwa haraka, na kutoa ripoti ya matokeo na mapendekezo yenye mashiko kwa Rais, ambaye atachukua hatua kulingana na mapendekezo hayo katika kipindi cha siku thelathini.
(7) Mtu atakayesimamishwa kazi chini ya Kifungu hiki ana haki ya kuendelea kupokea nusu ya zawadi na faida ya afisi akiwa amesimamishwa kazi.