(1) Pendekezo la marekebisho ya Katiba hii litatekelezwa kwa mujibu wa Kifungu cha 256 au 257, na kupitishwa kwa mujibu wa ibara ya (2) kwenye kura ya maamuzi, iwapo marekebisho hayo yanahusu suala lolote kati ya masuala yafuatayo–
- (a) mamlaka makuu ya Katiba;
- (b) mipaka ya Kenya;
- (c) mamlaka ya watu;
- (d) maadili ya kitaifa, kanuni za kiutawala zilizoorodheshwa katika Kifungu cha 10 (2) (a) hadi (d);
- (e) Sheria ya Haki;
- (f) kipindi cha kuhudumu cha Rais;
- (g) uhuru wa Idara ya Mahakama, Tume, na afisi huru zinazorejelewa katika Sura ya Kumi na tano;
- (h) majukumu ya Bunge;
- (i) malengo, kanuni na muundo wa serikali ya ugatuzi; au
- (j) masharti ya Sura hii,
(2) Pendekezo la marekebisho litapitishwa kwa kura ya maamuzi chini ya ibara ya (1) iwapo–
- (a) angalau asilimia ishirini ya wapiga kura waliosajiliwa katika angalau nusu ya idadi ya kaunti itapiga kura katika kura ya maamuzi; na
- (b) marekebisho yanaungwa mkono na wananchi wengi wanaopiga kura katika kura ya maamuzi.
(3) Marekebisho katika Katiba hii ambayo hayahusiani na yale yaliyofafanuliwa katika ibara ya (1) yataidhinishwa ama–
- (a) na Bunge, kulingana na Kifungu cha 256; au
- (b) na watu pamoja na Bunge, kulingana na Kifungu cha 257.