Ruka hadi Yaliyomo

(1) Mswada wa kurekebisha Katiba hii–

  • (a) unaweza kuwasilishwa katika mojawapo ya viwango vya Bunge;
  • (b) haupaswi kuangazia suala lolote jingine isipokuwa yale yanayotokana na marekebisho ya sheria katika Mswada huo;
  • (c ) hautafikishwa kusomwa kwa mara ya pili katika mojawapo ya vitengo vya Bunge, katika muda wa siku tisini baada ya kusomwa kwa Mswada kwa mara ya kwanza katika Bunge hilo; na
  • (d) utakuwa umepitishwa na Bunge wakati kila mojawapo ya vitengo vya Bunge kimepitisha Mswada huo katika kusomwa kwa mara ya pili na tatu, kwa idadi isiyopungua thuluthi mbili ya wabunge wote katika ngazi hiyo.

(2) Bunge litatangaza Mswada wowote wa kurekebisha Katiba hii, na kuandaa mjadala wa umma kuhusiana na Mswada huo.

(3) Baada ya Bunge kupitisha Mswada wa kurekebisha Katiba hii, Maspika wa viwango vyote viwili vya Bunge watawasilisha kwa pamoja kwa Rais–

  • (a) Mswada, kutiwa saini na kuchapishwa; na
  • (b) cheti kwamba Mswada huo umepitishwa na Bunge kwa mujibu wa Kifungu hiki.

(4) Kulingana na ibara ya (5), Rais atautia sahihi Mswada huo na kuufanya uchapishwe katika muda wa siku thelathini baada ya Mswada huo kuidhinishwa na Bunge.

(5) Iwapo Mswada wa kurekebisha Katiba hii unapendekeza marekebisho yanayotajwa katika katika Kifungu cha 255 (1)–

  • (a) kabla ya Rais kuutia sahihi Mswada huo, ataiomba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kufanya kura ya maamuzi ya kitaifa katika muda wa siku tisini ili kuidhinisha Mswada huo; na
  • (b) katika muda wa siku thelathini baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka kumthibitishia Rais kwamba Mswada huo umepitishwa kulingana na Kifungu cha 255 (2), Rais atautia sahihi Mswada huo na kuufanya uchapishwe.
Msimbo wa QR unaounganisha kwenye https://blog.afro.co.ke/sw/katiba/sura-16/kifungu-256/marekebisho-ya-juhudi-za-bunge/