(1) Katiba hii inatambua utamaduni kama msingi wa taifa na jumla ya ustaarabu wa watu na taifa la Kenya.
(2) Serikali–-
- (a) itakuza aina zote za kitaifa na kitamaduni za kujieleza kupitia fasihi, sanaa, sherehe za kitamaduni, sayansi, mawasiliano, habari, vyombo vya habari, uchapishaji, maktaba na turathi nyingine za kitamaduni;
- (b) itatambua jukumu la sayansi na teknolojia za kiasili katika maendeleo ya nchi;
- (c) itatambua haki za kiubunifu za watu wa Kenya;
(3) Bunge litatunga sheria–
- (a) kuhakikisha kwamba jamii zinapewa fidia au mrabaha kwa kutumiwa kwa turathi zao za kitamaduni; na
- (b) kutambua na kulinda umiliki wa mbegu na mimea mbalimbali ya kiasili, sifa tofauti za kimaumbile na matumizi yake miongoni mwa jamii za Kenya.