(1) Iwapo mtu amepata uraia kwa kusajiliwa, uraia huo unaweza kupokonywa iwapo–
- (a) mtu huyo alijipatia uraia huo kwa njia ya ulaghai, udanganyifu wa uwakilishi au kuficha ukweli unaotakikana;
- (b) iwapo mtu huyo, katika vita vyovyote ambavyo Kenya ilihusika, kinyume na sheria alifanya biashara au kuwasiliana na adui au amejihusisha au kushiriki biashara na ambayo kwa kujua, ilitekelezwa kwa namna ambayo ilikuwa ni kusaidia adui;
- (c) katika kipindi cha miaka mitano baada ya kusajiliwa, amepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu au zaidi; au
- (d) wakati wowote ule baada ya kusajiliwa amepatikana na hatia ya uhaini au hatia ambayo–
- (i) amepewa adhabu ya kifungo cha angalau miaka saba au zaidi; au
- (ii) hukumu kali zaidi inaweza kutolewa.
(2) Uraia wa mtu ambaye alichukuliwa kuwa raia kwa kuzaliwa kama inavyofikiriwa katika Kifungu cha 14 (4) unaweza kupokonywa iwapo-
- (a) uraia ulipatikana kwa njia ya ulaghai, udanganyifu wa uwakilishi au kuficha ukweli unaotakikana kwa mtu yoyote;
- (b) utaifa au kuzaliwa kwa mtu huyo kunajulikana na kufichua kwamba mtu huyo alikuwa raia wa nchi nyingine; au
- (c) umri wa mtu huyo unakuja kujulikana na kufichua kwamba alikuwa na umri wa zaidi ya miaka minane alipopatikana nchini Kenya.