(1) Sheria ya Haki ni kiungo muhimu katika utawala wa kidemokrasia nchini Kenya na ndiyo msingi wa sera za kijamii, kiuchumi na kitamaduni.
(2) Lengo la kutambua na kulinda haki za binadamu na uhuru wa kimsingi ni kulinda heshima ya watu binafsi na jamii tofauti na kukuza haki za kijamii na kufanikisha uwezo wa binadamu wote.
(3) Haki na uhuru wa kimsingi zinazotajwa katika sura hii–
- (a) ni za kila mtu binafsi na wala hazikabidhiwi na Serikali;
- (b) hazitengi haki na uhuru mwingine wa kimsingi ambao haukutajwa katika Sura hii, lakini zinazotambuliwa na kukubaliwa na sheria, ila kwa kiwango ambacho hazikubaliani na Sura hii; na
- (c) zinazingatia mipaka inayoelezwa katika Katiba hii.