(1) Sheria ya Haki inahusu sheria zote na inajumlisha idara zote za Serikali na watu wote.
(2) Kila mtu ana haki na uhuru wa kimsingi uliotajwa katika Sheria ya Haki, kwa kiwango kikubwa kuambatana na hali ya haki hiyo au uhuru huo wa kimsingi.
(3) Katika kutekeleza Sheria ya Haki, mahakama inapaswa–
- (a) kukuza sheria kupita kiwango ambacho sheria imeiangazia haki au uhuru wowote wa kimsingi; na
- (b) kuchukua fasiri inayopendelea kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa haki au uhuru wa kimsingi.
(4) Katika kufasiri Sheria ya Haki, mahakama, mahakama maalum, au mamlaka nyingine zitaendeleza–
- (a) maadili yanayoongoza jamii iliyo wazi na ya kidemokrasia kulingana na heshima ya ubinadamu, ulinganifu, usawa, na uhuru; na
- (b) imani, madhumuni na malengo ya Sheria ya Haki.
(5) Katika utekelezaji wa haki yoyote chini ya Kifungu cha 43, endapo Serikali inadai kuwa haina rasilimali za kutekeleza haki hiyo, mahakama, mahakama maalum au mamlaka yoyote itaongozwa na kanuni zifuatazo-
- (a) ni jukumu la Serikali kuonyesha kuwa rasilmali hazipo;
- (b) katika kugawa rasilmali, Serikali ina jukumu la kuhakikisha kuna uwezekano mkubwa wa kunufaishwaa na haki au uhuru wa kimsingi kwa kuzingatia hali halisi, kukiwemo kutengwa kwa baadhi ya makundi au watu binafsi; na
- (c) Mahakama, mahakama maalum au mamlaka nyingine haziwezi kuingilia uamuzi wa idara ya Serikali kuhusu ugavi wa rasilmali zilizopo, hasa kwa misingi kuwa itakuwa imefikia uamuzi tofauti.