(1) Ni wajibu wa kimsingi wa Serikali na kila idara ya Serikal kuzingatia, kuheshimu, kulinda, kuendeleza, na kutimiza haki na uhuru wa kimsingi katika Sheria ya Haki.
(2) Serikali itachukua hatua za kisheria, kisera na nyinginezo ikihusisha uwekaji wa viwango ili kufanikisha ufikiaji wa haki kama ilivyohakikishiwa katika ibara ya 43.
(3) Ni wajibu wa mashirika yote ya Serikali na watumishi kushughulikia mahitaji ya makundi maalum katika jamii, wakiwemo wanawake, wazee, watu wenye ulemavu, watoto, vijana na jamii za walio wachache au zilizotengwa, pamoja na jamii fulani za kikabila, kidini na kitamaduni.
(4) Serikali itabuni na kutekeleza sheria ili kutimiza wajibu wake wa kimataifa kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kimsingi.