(1) Kila mtu ni sawa mbele ya sheria na ana haki ya kulindwa na kupata manufaa sawa ya sheria.
(2) Usawa unajumuisha kupata haki na uhuru wote wa kimsingi kwa njia iliyo kamili na sawa.
(3) Wanawake na wanaume wana haki ya usawa ikiwemo haki ya kupata nafasi sawa katika shughuli za kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kijamii.
(4) Serikali, kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja, haitakuwa na ubaguzi dhidi ya mtu yeyote kwa misingi yoyote ikiwemo asili, jinsia, ujauzito, hali ya mtu kindoa, hali ya kiafya, asili ya kikabila au kijamii, rangi, umri, ulemavu, dini, dhamiri, imani, utamaduni, mavazi, lugha au kuzaliwa.
(5) Mtu hatakuwa na ubaguzi dhidi ya mwingine kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo katika misingi iliyotajwa na kuonyeshwa na ibara ya (4).
(6) Ili kutoa athari kamilifu za kutimiza haki zinazohakikishiwa na Kifungu hiki, Serikali itachukua hatua za kisheria na nyinginezo kukiwemo vitendo sawazishi na sera ambazo zimebuniwa kupinga athari za kutonufaika kwa watu binafsi au makundi ya watu kwa sababu ya ubaguzi wa hapo awali.
(7) Hatua yoyote inayochukuliwa chini ya ibara ya (6) itashughulikia kikamilifu fidia yoyote kwa kuzingatia uhitaji ulioko .
(8) Pamoja na hatua zinazokusudiwa katika ibara ya (6), Serikali itachukua hatua za kisheria na nyinginezo ili kutekeleza kanuni kwamba, idadi ya watu waliochaguliwa au kuteuliwa katika mashirika haitakuwa na wanachama zaidi ya thuluthi mbili wa jinsia moja.