Ruka hadi Yaliyomo

(1) Kila mwananchi ana uhuru wa kuwa na uchaguzi wa kisiasa, ikiwemo haki ya-–

  • (a) kuunda, au kushiriki katika uundaji wa chama cha kisiasa;
  • (b) kushiriki katika shughuli za, au kusajili wanachama kwa niaba ya chama cha kisiasa; au
  • (c) kufanyia kampeni chama cha kisiasa.

(2) Kila mwananchi ana haki ya kushiriki katika uchaguzi huru, wa haki na unaofanyika mara kwa mara kwa misingi ya haki ya kupiga kura kwa wote na uhuru wa hiari ya mpiga kura kwa–

  • (a) shirika au afisi yoyote ya umma iliyobuniwa chini ya Katiba hii na inayofanya uchaguzi; na
  • (b) kiongozi wa afisi yoyote ya chama cha kisiasa ambacho mwananchi huyo ni mwanachama.

(3) Kila raia akiwa mtu mzima ana haki pasipo na masharti yasiyo na busara–

  • (a) kujiandikisha kama mpiga kura;
  • (b) kupiga kura ya siri katika uchaguzi wowote au katika kura ya maamuzi; na
  • (c) kugombea wadhifa katika afisi ya umma, au afisi katika chama cha kisiasa ambacho yeye ni mwanachama na endapo atachaguliwa, ashike usukani.
Msimbo wa QR unaounganisha kwenye https://blog.afro.co.ke/sw/katiba/sura-4/sehemu-2/kifungu-38/haki-za-kisiasa/