Ruka hadi Yaliyomo

(1) Kila mtu aliyetiwa mbaroni ana haki ya–

  • (a) kuarifiwa kwa upole na kwa lugha anayoielewa, kuhusu–
    • (i) sababu ya kukamatwa;
    • (ii) haki ya kunyamaza; na
    • (iii) matokeo ya kutonyamaza;
  • (b) kunyamaza;
  • (c) kuwasiliana na wakili na watu wengine ambao msaada wao unahitajika;
  • (d) kutolazimishwa kutubu au kukiri hatia, hali ambayo inaweza kutumiwa katika ushahidi dhidi yake;
  • (e) kutenganishwa na watu wanaohudumia vifungo;
  • (f) kufikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo, lakini si baada ya–
    • (i) saa ishirini na nne baada ya kukamatwa; au
    • (ii) iwapo hizo saa ishirini na nne zimekamilika wakati ambapo vikao vya mahakama haviendelei au kwa siku isiyo ya mahakama, kufikia mwisho wa siku ya mahakama inayofuatia;
  • (g) kufunguliwa mashtaka au kuarifiwa kuhusu sababu ya kuendelea kuzuiliwa kwake, au kuachiliwa huru siku yake ya kwanza ya kufikishwa mahakamani; na
  • (h) kuachiliwa kwa dhamana kwa sababu zinazoeleweka kabla ya kushtakiwa isipokuwa kukiwa na sababu nyingine za kulazimisha kutendwa kinyume cha dhamana hiyo.

(2) Mtu hatawekwa rumande kwa kosa linaloweza kuadhibiwa kwa kutozwa faini pekee au kufungwa gerezani kwa muda usiozidi miezi sita.

Msimbo wa QR unaounganisha kwenye https://blog.afro.co.ke/sw/katiba/sura-4/sehemu-2/kifungu-49/waliotiwa-mbaroni/