Ruka hadi Yaliyomo

(1) Kila mtu ana haki ya kutaka mzozo wowote unaoweza kusuluhishwa kisheria kuamuliwa katika kikao cha haki mahakamani au, ikiwezekana asasi au mahakama maalum iliyo huru na isiyoegemea upande wowote.

(2) Kila mshtakiwa ana haki ya kesi yake kusikizwa kwa njia ya haki, ikiwemo haki ya–

  • (a) kuaminiwa kutokuwa na hatia hadi ithibitishwe kinyume;
  • (b) kuarifiwa kuhusu mashtaka na kupewa taarifa ya kutosha kuyahusu;
  • (c) kuwa na wakati na vifaa vya kutosha kutayarisha nyenzo za kujitetea;
  • (d) kushtakiwa kwenye mahakama ya umma iliyobuniwa kwa mujibu wa Katiba hii;
  • (e) kuanzishwa na kumalizika kwa mashtaka bila kucheleweshwa;
  • (f) kuwepo wakati wa kesi isipokuwa pale ambapo mienendo ya mshtakiwa inatatiza vikao vya kesi hiyo;
  • (g) kuchagua na kuwakilishwa na wakili na kuelezwa kuhusu haki hii moja kwa moja;
  • (h) kuwa na wakili aliyetolewa na Serikali kwa gharama ya Serikali yenyewe, endapo haki yake ya msingi imevunjwa, na aarifiwe kuhusu haki hii moja kwa moja;
  • (i) kunyamaza, na kutotoa ushahidi wakati wa kesi;
  • (j) kuelezwa mwanzoni kuhusu ushahidi ambao kiongozi wa mashtaka ananuia kutumia na kuweza kuufikia ushahidi huo.
  • (k) kuleta na kupinga ushahidi;
  • (l) kutolazimishwa kutoa ushahidi wa kujifunga;
  • (m) kuwa na usaidizi wa mkalimani bila ya kulipishwa endapo mshtakiwa hawezi kuelewa lugha inayotumiwa katika kesi;
  • (n) kutohukumiwa kwa kitendo, au kosa ambalo wakati wa utendekaji au ukosaji halikuwa–
    • (i) kosa nchini Kenya; au
    • (ii) kosa la jinai chini ya sheria ya kimataifa;
  • (o) kutoshtakiwa kwa kosa la kulinganishwa na tendo au kosa ambalo mtu huyo amewahi ama kuachiliwa au kuhukumiwa kwalo;
  • (p) kunufaika kwa angalau adhabu ndogo kabisa katika adhabu zilizoruhusiwa endapo adhabu iliyoidhinishwa kwa kosa lake imebadilishwa kati ya muda wa utendekaji wa kosa hilo na wakati wa kuhukumiwa; na
  • (q) kukata rufani au kuchunguzwa upya kwa kesi hiyo na mahakama ya ngazi ya juu.

(3) Kila kifungu hiki kinapohitaji taarifa kutolewa kwa mtu, taarifa hiyo itatolewa katika lugha anayoielewa mtu huyo.

(4) Ushahidi unaopatikana katika njia inayokiuka haki yoyote au uhuru wowote wa kimsingi uliotolewa katika Sheria ya Haki utaachwa endapo utekelezaji wa ushahidi huo utafanya kesi kukosa haki au uwe kikwazo katika upatikanaji wa haki.

(5) Mshtakiwa–

  • (a) anayeshtakiwa kwa kosa fulani, kando na kosa ambalo mahakama inaweza kukamilisha kwa haraka, atakuwa na ruhusa endapo ataomba, ya kupata nakala ya rekodi za kesi.
  • (b) ana haki ya kupata nakala ya rekodi ya kesi ya vikao vya mashtaka kwa wakati unaofaa baada ya kukamilishwa kwa kesi hiyo, kwa malipo fulani kama inavyoidhinishwa na sheria.

(6) Mtu aliyehukumiwa kwa kosa la jinai anaweza kulalamikia mahakama kuu ili kusikizwa upya kwa kesi iwapo–

  • (a) rufani yake imetupiliwa mbali na mahakama ya ngazi za juu ambayo mtu huyo alikuwa na haki ya kukata rufani, au awe hakukata rufani katika muda unaoruhusiwa kufanya hivyo; na
  • (b) ushahidi mpya na wa kushawishi umepatikana.

(7) Ili kutimiza haki, mahakama inaweza kuruhusu msuluhishi kusaidia mlalamishi au mshtakiwa kuwasiliana na mahakama.

(8) Kifungu hiki hakikatazi kuzuiwa kwa vyombo vya habari ama umma kutokuwa mahakamani, kama kuzuiwa huko ni muhimu, katika jamii huru na ya kidemokrasia, ili kuwalinda mashahidi, wanyonge, maadili, utulivu wa umma, ama usalama wa kitaifa.

(9) Bunge litatunga sheria ya kutoa ulinzi, haki na hali ya waathiriwa wa hatia.

Msimbo wa QR unaounganisha kwenye https://blog.afro.co.ke/sw/katiba/sura-4/sehemu-2/kifungu-50/kusikizwa-kesi/