(1) Hali ya hatari inaweza kutangazwa tu kwa kuzingatia Kifungu cha 132 (4) (d) na pale tu–
- (a) Nchi inatishiwa na vita, uvamizi, upinzani mkubwa, vurugu, janga la kitaifa au dharura zingine za umma; na
- (b) tangazo hilo ni muhimu katika kukabiliana na hali ya hatari iliyotangazwa.
(2) Tangazo la hali ya hatari, na sheria yoyote itakayotungwa au hatua nyingine itakayochukuliwa kutokana na tangazo hilo, itatekelezeka tu–
- (a) kwa matazamio; na
- (b) kwa muda usiozidi siku kumi na nne kutoka siku ya kutangazwa kwa hali hiyo ya hatari, isipokuwa Baraza Kuu la Kitaifa liamue kuendeleza tangazo hilo.
(3) Baraza Kuu la Kitaifa linaweza kuendeleza tangazo la hali ya hatari–
- (a) kutokana na uamuzi uliochukuliwa-
- (i) kufuatia mijadala ya wazi Bungeni; na
- (ii) idadi kubwa ya wabunge kama inavyodokezwa katika ibara Ya (4); na
- (b) kwa muda usiozidi miezi miwili kwa wakati mmoja.
(4) Nyongeza ya kwanza ya kipindi cha hali ya hatari inahitaji kuungwa mkono na thuluthi mbili ya kura za wabunge, na itakayofuatia inahitaji kuungwa mkono na angalau robo tatu ya wabunge.
(5) Mahakama ya Juu inaweza kuamua kuhusu kufaa kwa–
- (a) tangazo la hali ya hatari;
- (b) nyongeza yoyote ya muda wa tangazo la hali ya hatari; na
- (c) sheria yoyote itakayotungwa au hatua yoyote nyingine itakayochukuliwa, kwa sababu ya tangazo la hali ya hatari.
(6) Sheria yoyote inayotungwa kwa sababu ya tangazo la hali ya hatari–
- (a) inaweza kuzuia uhuru wa kimsingi ulio katika Sheria ya Haki iwapo tu ni kwa kiwango kwamba–
- (i) uzuiaji huo unastahili kutokana na dharura hiyo; na
- (ii) sheria hiyo inaambatana na majukumu ya Jamhuri chini ya sheria ya kimataifa kuhusiana na hali ya hatari.
- (b) Haitatekelezwa hadi ichapishwe kwenye Gazeti rasmi la serikali.
(7) Tangazo la hali ya hatari au sheria inayotungwa au hatua yoyote nyingine inayochukuliwa kwa sababu ya tangazo lolote, haitaruhusu au kuidhinisha kufidia kwa Serikali au mtu yeyote kwa misingi ya tendo lolote la ukiukaji wa sheria.