Ruka hadi Yaliyomo

(1) Tume ya Haki za Kibinadamu na Usawa imeundwa.

(2) Majukumu ya Tume hii ni–

  • (a) kuendeleza kuheshimika kwa haki za binadamu na kuendeleza utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu katika Jamhuri;
  • (b) kuendeleza usawa wa kijinsia na usawazishaji kwa jumla, kuratibu na kuhakikisha jinsia imezingatiwa katika maendeleo ya kitaifa;
  • (c) kuimarisha na kulinda uzingativu wa haki za binadamu katika taasisi za umma na za kibinafsi;
  • (d) kufuatilia, kuchunguza na kuripoti uzingativu wa haki za binadamu katika nyanja zote za kitaifa zikiwemo idara za usalama wa kitaifa;
  • (e) kupokea na kuchunguza malalamiko kuhusu tuhuma za ukiukaji wa haki na hivyo basi kuchukua hatua za kupata marekebisho yanayofaa pale ambapo haki za binadamu zimekiukwa;
  • (f) kwa juhudi zake au kwa misingi ya malalamiko, kuchunguza au kutafiti juu ya haki za binadamu, na kutoa mapendekezo ya kuimarisha utendakazi wa mashirika ya Serikali;
  • (g) kuwa kama chombo kikuu cha Serikali katika kuhakikisha uzingativu wa majukumu yaliyo chini ya maagano na mikataba inayohusu haki za binadamu;
  • (h) kuchunguza mienendo yoyote katika masuala ya serikali, au kitendo au kosa katika utawala wa umma katika nyanja zote za serikali zinazotuhumiwa au kushukiwa kudhulumu au kutofaa, na kupelekea utovu wa nidhamu au dhuluma;
  • (i) kuchunguza malalamiko yoyote kuhusu mienendo ya afisa ambayo ni pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka, matendo mabaya, dhihirisho la kutotenda haki au kuvunja sheria, au kunyanyasa, na kutoshughulika;
  • (j) kuripoti malalamiko yaliyochunguzwa katika aya ya (h) na (i) na kuchukua hatua za kurekebisha;
  • (k) kutekeleza jukumu lingine lolote linaloagizwa na sheria.

(3) kila mtu ana haki ya kulalamika kwa tume akidai kwamba haki na uhuru wa kimsingi katika Sheria ya Haki zimenyimwa, zimekiukwa, zimevunjwa au kutishiwa.

(4) Bunge litatunga sheria kutoa uwezo kamili wa sehemu hii, na sheria nyingine yoyote kama hii inaweza kupanga upya Tume hii na kuzifanya kuwa mbili au zaidi zilizotenganishwa.

(5) Iwapo Bunge litatunga sheria ya kupanga upya Tume chini ya ibara ya (4)–

  • (a) sheria hiyo itagawa kila jukumu la Tume iliyotajwa katika Kifungu hiki kwa tume moja au nyingine zinazoirithi.
  • (b) kila mojawapo ya tume hizi zilizorithi, itakuwa na mamlaka sawa na ile ya Tume ambayo imetajwa katika Kifungu hiki; na
  • (c) kila tume iliyorithi itakuwa tume kwa maana ya iliyoko katika Sura ya Kumi na Tano, na itakuwa na hadhi na mamlaka sawa na tume zilizo chini ya Sura hii.
Msimbo wa QR unaounganisha kwenye https://blog.afro.co.ke/sw/katiba/sura-4/sehemu-5/kifungu-59/tume-ya-haki/