(1) Ardhi nchini Kenya itashikiliwa, kutumiwa na kusimamiwa katika misingi ya usawa, ufanisi, uzalishaji na uendelevu, na kwa mujibu kanuni zifuatazo-
- (a) uwezo sawa wa kupata ardhi;
- (b) usalama wa haki za ardhi;
- (c) usimamizi endelevu na wa manufaa, wa rasilmali za ardhi;
- (d) usimamizi wa ardhi kwa uwazi na kwa gharama ya kufaa;
- (e) hifadhi na utunzaji bora wa maeneo muhimu kiekolojia;
- (f) kumaliza ubaguzi wa kijinsia katika sheria, mila na desturi zinazohusiana na mali iliyomo katika ardhi hiyo; na
- (g) kuhimiza jamii kutatua mizozo kuhusu ardhi kupitia mifumo ya kiasili inayoambatana na Katiba hii.
(2) Kanuni hizi zitatekelezwa kupitia kwa sera ya ardhi ya kitaifa inayoundwa na kuchunguzwa upya kila mara na serikali ya kitaifa kupitia kwa sheria.