(1) Ardhi ya umma ni–
- (a) ardhi ambayo wakati wa kuanza kutumika kwa Katiba hii ni mali ya Serikali inavyoelezwa na Sheria ya Bunge wakati huo;
- (b) ardhi inayomilikiwa, kutumiwa au kukaliwa kisheria na taasisi yoyote ya Serikali, isipokuwa pale ambapo ardhi hiyo inakaliwa na idara ya Serikali chini ya kukodi kibinafsi;
- (c) ardhi iliyokabidhiwa Serikali kwa njia ya kuuza, kurudishiwa au kusalimishwa;
- (d) ardhi ambayo haimilikiwi kisheria na mtu yeyote au jamii yoyote;
- (e) ardhi ambayo mrithi wake hawezi kutambuliwa kwa vyovyote kisheria;
- (f) ardhi yoyote iliyo na madini au mafuta inavyoelezwa kisheria;
- (g) misitu ya Serikali kando na misitu inayotajwa katika Kifungu cha 63 (2) (d) (i), hifadhi ya wanyama, chemichemi za maji, mbuga za kitaifa, hifadhi za wanyama za serikali na sehemu maalum zilizolindwa;
- (h) barabara zote kulingana na Sheria ya Bunge;
- (i) mito yote, maziwa yote na sehemu nyingine za maji kama inavyoelezwa na Sheria ya Bunge;
- (j) mipaka ya bahari, maeneo maalum ya kiuchumi na chini ya bahari;
- (k) miamba ya kibara;
- (l) ardhi yote kati ya nyanda za juu na za chini za maji;
- (m) ardhi yoyote ambayo haijaainishwa kama ya kibinafsi au ya jamii chini ya Katiba hii; na
- (n) ardhi yoyote itakayotangazwa kuwa ya umma na Sheria ya Bunge–
- (i) itakayotumika katika tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii; na
- (ii) iliyoidhinishwa baada ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.
(2) Ardhi ya umma itatolewa na kumilikiwa na Serikali ya Kaunti kwa amana kwa niaba ya wakazi wa Kaunti hiyo na itasimamiwa kwa niaba yao na Tume ya Kitaifa ya Ardhi iwapo imeainishwa chini ya–
- (a) ibara ya (1) (a),(c), (d) au (e); na
- (b) ibara ya (1)(b) mbali na ardhi inayoshikiliwa, inayotumiwa au inayomilikiwa na idara za Serikali ya kitaifa.
(3) Ardhi ya umma, inayoainishwa chini ya ibara ya (1) (f) hadi (m) itatolewa na kumilikiwa na Serikali ya kitaifa kwa amana kwa niaba ya wananchi wa Kenya na itasimamiwa kwa niaba yao na Tume ya Kitaifa ya Ardhi.
(4) Ardhi ya umma haitatolewa au kutumiwa isipokuwa kwa kuzingatia Sheria ya Bunge inayofafanua hali na masharti ya kutolewa au matumizi hayo.