(1) Kila chama cha kisiasa–
- (a) kitakuwa na sifa za kitaifa kama inavyopendekezwa na Sheria ya Bunge;
- (b) kiwe na taasisi ya kiutawala iliyochaguliwa kidemokrasia;
- (c) kitadumisha na kukuza umoja wa kitaifa;
- (d) kitazingatia kanuni za kidemokrasia za utawala bora, kudumisha na kuendeleza demokrasia kupitia kwa uchaguzi wa mara kwa mara, ulio na haki na huru katika chama;
- (e) kitaheshimu haki za kila mtu ili kushiriki katika harakati za kisiasa, yakiwemo makundi ya walio wachache na wale waliotengwa;
- (f) kitaheshimu na kudumisha haki za binadamu na uhuru wa kimsingi, na usawa wa kijinsia na usawazishaji;
- (g) kitadumisha malengo na kanuni za Katiba hii na utawala wa sheria; na
- (h) kitazingatia kanuni za maadili ya vyama vya kisiasa.
(2) Chama cha kisiasa–
- (a) hakitabuniwa kwa misingi ya kidini, lugha, mbari, kabila, jinsia au kwa misingi ya kimaeneo au kujihusisha katika kampeni za kusambaza chuki na shihata katika misingi ya masuala mengine kama hayo;
- (b) hakitajihusisha na au kuchochea ghasia kwa, au vitisho kwa, wanachama wake, wafuasi, wapinzani au mtu mwingine yeyote;
- (c) hakitaanzisha au kufadhili vikosi vya jeshi la wanamgambo wa kuvizia, makundi haramu au mashirika mengine kama hayo;
- (d) hakitajihusisha katika utoaji hongo au aina nyingine za ufisadi; au
- (e) isipokuwa kwa jinsi ilivyoelezwa katika Sura hii au kwa mujibu wa Sheria ya Bunge, kukubali au kutumia rasilimali ya umma ili kuimarisha maslahi yake au wagombeaji wake katika uchaguzi