(1) Kutabuniwa Tume ya Huduma ya Bunge.
(2) Tume hii itawahusisha–
- (a) Spika wa Baraza la Kitaifa kama mwenyekiti;
- (b) Naibu mwenyekiti aliyechaguliwa na Tume kutoka kwa wanachama walioteuliwa kwa mujibu wa aya (c);
- (c) wanachama saba walioteuliwa na Bunge kutoka miongoni mwa wabunge ambao–
- (i) wanne watateuliwa kwa usawa kutoka Mabunge yote mawili na chama au washirika katika muungano unaobuni Serikali ya kitaifa na ambao wawili kati yao watakuwa wanawake; na
- (ii) watatu watakuwa wameteuliwa na vyama visivyo kwenye Serikali ya taifa, angalau mmoja wao atateuliwa kutoka kila Bunge, na angalau mmoja wao atakuwa mwanamke; na
- (d ) mwanamume na mwanamke walioteuliwa na Bunge kutoka miongoni mwa watu ambao si wabunge lakini wana uzoefu mkubwa katika masuala yanayohusu umma.
(3) Karani wa Seneti atakuwa katibu wa Tume hiyo.
(4) Mwanachama wa Tume atatoka afisini–
- (a) iwapo mtu huyo ni Mbunge-
- (i) baada ya kukamilika kwa kipindi cha Bunge ambacho mtu huyo alikuwa mbuge;
- (ii) iwapo mtu huyo anakoma kuwa Mbunge; au
- (b ) iwapo mtu huyo ni mbunge mteule, baada ya kufutiliwa mbali kwa uteuzi wake na Bunge.
(5) licha yai Ibara ya (3), baada ya kumalizika kwa kipindi cha Bunge, mwanachama wa Tume aliyeteuliwa kwa mujibu wa ibara ya (2) (c) ataendelea kuwa afisini hadi mwanachama mwingine atakapoteuliwa na Bunge ili kuchukua nafasi yake.
(6) Tume ina jukumu la–
- (a) kutoa huduma na kusaidia ili kufanikisha utendakazi bora wa Bunge;
- (b) kubuni afisi katika huduma ya Bunge, na kuteua na kuwasimamia wanaoshikilia nyadhifa afisini humo;
- (c) kutayarisha makadirio ya matumizi ya fedha za kila mwaka katika huduma za Baraza la Kitaifa na kudhibiti bajeti yake;
- (d) kuanzisha ama kibinafsi au kwa pamoja na mashirika husika, mipango ya kukuza maadili ya ya Bunge; na
- (e) kutekeleza majukumu mengine–
- (i) muhimu kwa manufaa ya wabunge na wafanyakazi wa Bunge; au
- (ii) yatakayopendekezwa na sheria ya kitaifa.