(1) Mwanachama wa Baraza la Kitaifa akiungwa mkono na robo ya idadi ya Wabunge wote anaweza kuwasilisha hoja Bungeni ya kuchunguzwa kwa uwezo wa afya ya kiakili au kimwili ya Rais katika kutekeleza majukumu ya afisi yake.
(2) Iwapo hoja iliyo kwenye ibara ya (1) itaungwa mkono na Wabunge walio wengi wa Bunge la Kitaifa–
- (a) Spika wa Bunge atamjulisha Jaji Mkuu kuhusu uamuzi huu katika kipindi cha siku mbili; na
- (b) Rais ataendelea kutekeleza majukumu ya afisi ikisubiriwa matokeo ya mashauri yanayohitajika katika Kifungu cha hiki.
(3) Jaji Mkuu katika kipindi cha siku saba, baada ya kupokea notisi ya uamuzi huu kutoka kwa Spika, atateua tume itakayokuwa na–
- (a) watu watatu ambao ni wataalamu katika kuendesha masuala ya matibabu chini ya sheria za Kenya, walioteuliwa na taasisi ambayo kwa kisheria inawajibika kuthibiti matendo ya taaluma ya tiba;
- (b) wakili mmoja wa Mahakama Kuu aliyeteuliwa na taasisi ambayo kisheria inawajibika kuthibiti matendo ya taaluma ya uwakili; na
- (c) mtu mmoja atakayeteuliwa na Rais.
(4) Iwapo Jaji Mkuu atashindwa kuteua tume chini ya ibara ya (3) , Naibu Jaji Mkuu atateua tume kama hii.
(5) Iwapo Rais atashindwa kumteua mtu wa tano, mtu huyu atateuliwa na–
- (a) mmoja wa familia ya Rais; au
- (b) pale ambapo hakuna yeyote wa familia anataka au kuweza kufanya uteuzi huo, ufanywe na mmoja aliye na uhusiano wa karibu na wa kidugu na Rais.
(6) Tume itachunguza suala hili na kuripoti kwa Jaji Mkuu na Spika wa Baraza la Kitaifa katika muda wa siku kumi na nne baada ya uteuzi.
(7) Spika wa Bunge atawasilisha ripoti hiyo ya tume kwa Baraza la Kitaifa katika kipindi cha muda wa siku saba baada ya kuipokea.
(8) Ripoti hiyo ya tume itakuwa ya mwisho na hakutakuwa na rufaa na ikiwa tume itaripoti kwamba Rais anaweza kutekeleza majukumu yake ya afisi, Spika wa Baraza la Kitaifa atatangaza katika Baraza la Kitaifa.
(9) Iwapo tume itatangaza kuwa Rais hawezi kutekeleleza majukumu ya afisi, Baraza la Kitaifa litapiga kura kuidhinisha ripoti hiyo.
(10) Iwapo wabunge walio wengi kati ya wabunge wote wa Baraza la Kitaifa watapiga kura kuunga mkono kuidhinisha ripoti hii, basi Rais wa ataondolewa mamlakani.