(1) Kutabuniwa afisi ya Mwanasheria Mkuu
(2) Mwanasheria Mkuu atapendekezwa na Rais na kwa idhini ya Baraza la Kitaifa, kuteuliwa na Rais.
(3) Sifa za kuteuliwa kwa Mwanasheria Mkuu ni sawa na zile za uteuzi wa Jaji Mkuu.
(4) Mwanasheria Mkuu–
- (a) ndiye mshauri mkuu kisheria kwa Serikali;
- (b) atawakilisha Serikali ya taifa mahakamani au katika kesi nyingine za kisheria ambazo Serikali ya Kitaifa inahusika, isipokuwa kesi za jinai; na
- (c) atatekeleza jukumu lingine lolote litakalotunukiwa afisi yake na kifungu cha Sheria ya Bunge au na Rais.
(5) Mwanasheria Mkuu atakuwa na mamlaka, kwa ruhusa ya mahakama , kuwa kama rafiki wa mahakama katika kesi za umma zile ambazo Serikali si mhusika.
(6) Mwanasheria Mkuu atakuza, kuhifadhi na kutetea utawala wa sheria na kulinda maslahi ya Jamhuri.
(7) Mamlaka ya Mwanasheria Mkuu yanaweza kutekelezwa na yeye mwenyewe au na wasaidizi katika afisi yake wakitekeleza majukumu hayo kulingana na maagizo maalum au ya kijumla.