(1) Kutabuniwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.
(2) Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atapendekezwa na Rais, na kwa idhini ya Baraza la Kitaifa, atateuliwa na Rais.
(3) Sifa za uteuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma zitakuwa sawa na zile za uteuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu.
(4) Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atakuwa na mamlaka ya kumwagiza Inspekta Mkuu wa Huduma ya Polisi ya Kenya kuchunguza habari yoyote au madai ya vitendo vya jinai, naye Inspekta Mkuu wa Huduma ya Polisi ya Kenya atatii maagizo hayo.
(5 ) Mkurugenzi wa mashtaka ya Umma atashikilia hatamu ya afisi yake kwa kipindi cha miaka nane na hatakuwa na nafasi ya kuteuliwa tena.
(6) Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atatekeleza mamlaka ya Taifa ya kuongoza mashtaka na anaweza–
- (a) Kuwasilisha na kuendeleza mashtaka ya kesi za uhalifu dhidi ya mtu yeyote katika mahakama yoyote (isipokuwa mahakama ya kijeshi) kutokana na kosa linalotuhumiwa kuwa limefanywa;
- (b) Kuchukua na kuendeleza kesi zozote ya uhalifu zilizowasilishwa katika mahakama yoyote (isipokuwa katika mahakama ya kijeshi) zilizowasilishwa na kuendelezwa na mtu mwingine au mamlaka; na
- (c) Kwa kutegemea ibara ya (7) na (8), kukomesha katika hatua yoyote, kabla ya hukumu kutolewa, kesi yoyote ya uhalifu iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma au kuchukuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya umma kulingana na aya (b)
(7) Pale ambapo kukomeshwa kwa kesi kunakorejelewa katika ibara ya (6)( c) kunapotekelezwa baada ya mshitakiwa kukamilisha kujitetea, mshitakiwa ataachiliwa huru.
(8) Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma hawezi kukomesha shitaka lolote bila ya idhini ya mahakama.
(9) Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaweza kuyaendesha yeye mwenyewe ama kumuagiza afisa wa afisi yake kulingana na masharti maalum au ya jumla.
(10) Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma hatahitaji idhini ya mtu au mamlaka yoyote kuwasilisha kesi za kijinai, na katika kutekeleza mamlaka au majukumu yake hataelekezwa au kudhibitiwa na mtu au mamlaka yoyote.
(11) Katika kutekeleza mamlaka yaliyotunukiwa na Kifungu hiki, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atazingatia maslahi ya taifa, maslahi ya utekelezaji wa haki na haja ya kuzuia na kuepuka matumizi mabaya ya utaratibu wa sheria.
(12) Bunge linaweza kutunga sheria ya kutunukia taasisi nyingine uwezo wa kuongoza mashtaka kuliko ile ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.