Kazi za MCA nchini Kenya ni za muhimu na za aina mbalimbali. MCA ni Mwanachama wa Baraza la Kaunti anayejulikana pia kama Mwakilishi wa Wadi.
Wanachama wa Baraza la Kaunti ni sehemu kuu ya serikali za kaunti na wanadumisha uwepo wa kaunti.
Mwanachama wa Baraza la Kaunti (MCA) ni mwakilishi aliyechaguliwa ambaye anasimamia kitengo cha uchaguzi kinachojulikana kama Wadi. Wadi ndicho kitengo kidogo zaidi cha uchaguzi (na kiutawala) kiikifuatiwa na Kaunti Ndogo (au Eneobunge), Kaunti na hatimaye Nchi.
MCA anawakilisha wakaazi wa kiwango cha Wadi katika Baraza la Kaunti. Wadi kadhaa huunda Kaunti Ndogo. Karani wa Baraza la Kaunti anafaa kuwaapisha Wanachama wa Baraza la Kaunti kwenye kikao cha kwanza cha Baraza hiyo.
Jedwali la Yaliyomo Onyesha/Ficha
Kazi za MCA
Kazi za MCA zile kuu ni kutunga sheria, uwakilishi, na uangalizi. Isitoshe, Sheria ya Serikali za Kaunti inabainisha majukumu ya Wanachama wa Baraza la Kaunti chini ya Kifungu cha 9.
Kazi za MCA aliyependekezwa nchini Kenya ni sawa na kazi za MCA aliyechaguliwa.
1. Kudumisha Mawasiliano ya Karibu na Wapiga Kura
MCA anapaswa kudumisha mawasiliano ya karibu na wapiga kura. Anapaswa kushauriana nao kuhusu masuala chini ya au yanayojadiliwa katika baraza la Kaunti.
Hii ina maana kwamba Wanachama wa Baraza la Kaunti hawapaswi ‘kutoweka’ mara baada ya kuchaguliwa na kujitokeza tena miaka mitano baadaye wakitafuta kura.
Wanapaswa kujitahidi kuwa na mawasiliano ya karibu na wale waliowachagua na kupatikana wakati watu wanawahitaji na waweze kufikiwa kwa urahisi.
Tafiti nyingi za umma kwa kawaida zinaonyesha kuwa Wakenya hutangamana na Wanachama wao wa Baraza la Kaunti zaidi ikilinganishwa na wawakilishi wengine waliochaguliwa. Hii ina maana kwamba imani ya umma kwao ni kubwa.
Wanachama hawa wanapaswa kujitahidi kuwafahamisha wapiga kura wao kuhusu masuala yaliyo mbele ya Baraza. Kisha wanapaswa kushauriana na wapiga kura wao na kuyapigia kura masuala haya kulingana na maoni ya wananchi.
2. Kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Wapiga kura kwa Baraza la Kaunti
Ni jukumu la MCA kuwakilisha wananchi. Kwa kufanya hivyo, anapaswa kuwasilisha maoni na mapendekezo ya watu mbele ya Baraza la Kaunti.
Kenya ni demokrasia isiyo ya moja kwa moja ambapo umma huchagua watu wachache kuzungumza kwa ajili ya walio wengi.
Baada ya mashauriano, Wanachama wa Baraza la Kaunti wanafaa kuwasilisha matakwa ya wananchi mbele ya Baraza hilo. Matakwa haya yanatofautiana katika Wadi zote na kila MCA anapaswa kutanguliza mahitaji ya Wadi yake.
Mapendekezo yanaweza kuwa katika mfumo wa miradi ya kipaumbele kama ile iliyo chini ya Hazina wa Maendeleo ya Wadi.
Mchakato wa Bajeti nchini Kenya pia huwapa fursa Wanachama kuwasilisha matakwa ya watu mbele ya Baraza. Mchakato huo unawapa fursa ya kuamua ugawaji wa rasilimali kwa kaunti.
Njia nyingine ambapo Wanachama wanaweza kuwasilisha matakwa ya watu ni kupitia sheria katika Baraza la Kaunti ikijumuisha hoja, mijadala na maazimio.
3. Kuhudhuria Vikao vya Baraza la Kaunti na Kamati zake
Jukumu hili la MCA ni muhimu sana. Wanachama hawawezi kuwasilisha maoni na mapendekezo ya watu ikiwa hawatahudhuria vikao vya Baraza la Kaunti.
Shughuli muhimu zaidi ya Baraza hufanyika katika kamati ambapo Wanachama hufanya mijadala mingi.
Ikiwa MCA yeyote atakosa kuhudhuria vikao vinane mfululizo vya Baraza la Kaunti, anaweza kupoteza kiti chake.
Vikao vya jumla na vya kamati ndio njia ambazo Wanachama wanaweza kutoa sauti zao. Wanaweza kutoa maoni yao kuhusu masuala yanayoathiri Wadi yao kupitia vikao vya jumla na kuyapigia kura masuala hayo.
Katika vikao vya kamati, wana jukumu la moja kwa moja katika kuwezesha ushirikishwaji wa umma na kuhalalisha shughuli za Baraza. Wanaweza kujua ukweli wa kesi, kuwachunguza mashahidi, kuchuja ushahidi, na kufanya hitimisho la kimantiki kuhusu masuala kadhaa mbele ya Baraza.
Kamati zinaruhusu maoni ya wananchi katika mchakato wa kutunga sheria za Baraza. Pia zinatumika kama njia za uangalizi.
Kamati hulisaidia Baraza katika kazi zake za kutunga sheria, kufuatilia na kupitia sheria, utawala na matumizi ya fedha, kukusanya taarifa na kutangaza masuala.
Wanachama wengine huhudhuria tu vikao vya kamati ili kupata marupurupu lakini sio na nia ya kuwakilisha wananchi. Kuhudhuria vikao isiwe mazoea bali Wanachama wafanye hivyo ili kuwatumikia wananchi.
4. Kutoa Uhusiano Kati ya Baraza la Kaunti na Wapiga kura kuhusu Utoaji wa Huduma za Umma
Serikali za Kaunti hutoa huduma muhimu za umma, kama vile afya, kilimo, maji na elimu ya awali. Watu wanajali huduma za umma na wanategemea serikali za kaunti kuziwasilisha ipasavyo.
Utoaji wa Huduma kwa Umma: Ni utaratibu ambao huduma za umma zinatolewa kwa umma na serikali za mitaa, manispaa au shirikisho.
Wanachama wanapaswa kujenga uhusiano kati ya Baraza la Kaunti na umma kuhusu utoaji wa huduma za umma. Jukumu hili la Wanachama wa Baraza la Kaunti linahusiana sana na kutunga sheria na uangalizi.
Kupitia sheria, Wanachama huamua jinsi serikali ya kaunti inavyogawa rasilimali za umma ndani ya kaunti. Wanapaswa kuhakikisha kuwa huduma za umma zimegawanywa kwa njia inayoheshimu usawa ndani ya kaunti.
Kupitia jukumu la uangalizi, wananchi wanaweka imani yao kwa Wanachama kuhakikisha kwamba walio na mamlaka kuu ya kaunti wanatekeleza sera na miradi ya kaunti kwa njia mwafaka.
Wanachama wana jukumu muhimu la kuhakikisha kuwa serikali ya kaunti inatoa huduma moja kwa moja hadi mashinani na kuhakikisha kuna pesa za kutosha kwa utoaji wa huduma (hizi).
Wanachama pia hujenga uhusiano kwa kushauriana na wapiga kura wao. Baraza la Kaunti hupanga mikutano ya hadhara kutafuta maoni ya umma kuhusu mipango na sera za serikali ya kaunti. Aidha, kwa kuwasilisha maoni ya umma mbele ya Baraza, MCA hurahisisha uhusiano huu.
Wanachama pia huhamasisha wakazi kutambua miradi ya kipaumbele kwa serikali ya kaunti kutekeleza, na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma.
Isitoshe, ni wajibu wa Wanachama kuwezesha elimu ya raia kuhusu jukumu la Baraza la Kaunti katika utoaji wa huduma kwa umma.
5. Kuongeza Maarifa ya Kitaalamu, Uzoefu au Maarifa Maalumu kwa Suala Lolote la Majadiliano katika Baraza la Kaunti.
Jukumu la Wanachama wa Baraza la Kaunti limekuwa likichunguzwa kila mara. Wanakabiliwa na ukosoaji wa kila mara kwa kukosa maarifa (ya kitaalamu) na tajriba ya kuendesha masuala ya Baraza la Kaunti.
Hapo awali, wengi wao hawakuweza kushiriki katika mijadala ya Baraza au kutunga sheria ambazo hazikuchunguzwa. Kulikuwa na idadi nzuri kati yao ambao kiwango cha elimu kilikuwa cheti cha msingi au shule ya upili tu. Wengine kadhaa walikuwa wameacha shule.
Licha ya hayo, Wanachama wanapaswa kutumia sifa zao za kitaaluma na ujuzi maalum kuendesha shughuli ya Baraza la Kaunti. Ujuzi huu ni muhimu, haswa katika kamati.
Kwa hivyo, ni muhimu kwa MCA kuwa na ujuzi wa masuala ya ndani ya kaunti na kitaifa huku pia akifuatilia mambo ya sasa. Baada ya yote, Wanachaa wanafanya na kutekeleza mabadiliko ambayo yatakuwa na athari halisi kwa maisha ya wale walio ndani ya kaunti wanayohudumu.
Maarifa ya kitaaluma, uzoefu, au ujuzi maalum ni muhimu kwa MCA yoyote kwa kuzalisha na kusimamia mipango na sera zinazotekelezeka.
Ustadi na uzoefu wanaopata katika sekta ya kibinafsi au ya umma kabla ya kutafuta ofisi ya umma unapaswa kutafsiri kwa masuala muhimu na maendeleo ya sera katika siasa (za Baraza).
Kile ambacho Wanachama wa Baraza la Kaunti hawapaswi kufanya
Jukumu la Wanachama wa Baraza la Kaunti linajizuia kwa mamlaka iliyotolewa na sheria. Mwanachama hapaswi kuhusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika masuala yafuatayo.
1. Majukumu ya utendaji ya Serikali ya Kaunti na usimamizi wake
Wanachama hawafai kutekeleza majukumu ya utendaji. Majukumu haya ni pamoja na usimamizi na utekelezaji wa fedha na utekelezaji wa miradi.
Wanachama wamezuiliwa kutekeleza majukumu ya kiutendaji kutokana na kanuni ya mgawanyo wa mamlaka na pia kuepuka mgongano wa kimaslahi.
Mgawanyo wa mamlaka, kwa hiyo, unarejelea mgawanyo wa majukumu ya serikali katika matawi tofauti ili kuzuia tawi lolote kutekeleza majukumu ya msingi ya lingine. Kusudi ni kuzuia mkusanyiko wa nguvu…
Hebu tutumie mfano wa Hazina ya Maendeleo ya Wadi ambayo Wanachama wa Baraza la Kaunti wanatamani sana kumiliki.
Ni jukumu la Baraza la Kaunti kuidhinisha matumizi ya umma. Kwa hiyo, Wanachama wakitenga fedha kwa ajili ya Hazina ya Wadi na bado wakasimamia na kutekeleza hazina hiyo, itakuwa vigumu kwao kuwajibikia jinsi hazina ilivyotumika kwa vile watakuwa wanajitia hatiani.
2. Utoaji wa huduma kana kwamba mwanachama ni afisa au mfanyakazi wa Serikali ya Kaunti
Wanachama hawafai kutekeleza majukumu yoyote kana kwamba ni wafanyikazi wa kaunti. Hii inatumika kwa Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti na Bodi ya Huduma za Baraza la Kaunti.
Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti inasimamia kuajiri na kusimamia wafanyikazi wa kaunti huku Bodi ya Huduma za Baraza la Kaunti ikifanya vivyo hivyo katika Baraza la Kaunti.
Kwa ufupi, jukumu la Wanachama wa Baraza la Kaunti halihusishi utoaji wa huduma za umma. Wao hutoa tu uhusiano katika utoaji wa huduma kati ya umma na serikali ya kaunti.
Kwa hivyo, kazi za MCA au majukumu ya MCA yanaweza kufupishwa kama kutunga sheria, uwakilishi na uangalizi (ikiwemo ugawaji wa bajeti).