Kifungu cha 152 cha Katiba ya Kenya kinabainisha kuwa Rais atawapendekeza na kwa idhini ya Baraza la Kitaifa kuwateua MaWaziri.
Waziri hatakuwa Mbunge.
Ofisi ya Waziri itakuwa wazi ikiwa Waziri–
- ameweza kujiuzulu kwa kuwasilisha kwa Rais taarifa iliyoandikwa ya kujiuzulu kwake;
- ameachishwa kazi na Rais; au
- ameachishwa kazi na Rais kufuatia mjadala uliopitishwa na Baraza la Kitaifa wa kumtaka Rais amwachishe kazi Waziri.
Jedwali la Yaliyomo Onyesha/Ficha
Kuondolewa Afisini kwa Waziri
Kifungu cha 152 (6) cha Katiba kinabainisha kuwa Mwanachama wa Baraza la Kitaifa anayeungwa mkono na angalau robo moja ya wabunge wote, anaweza kupendekeza mjadala wa kumtaka Rais amwachishe kazi Waziri.
Misingi ya kuondolewa afisini kwa Waziri
Waziri anaweza kuondolewa afisini kwa misingi ifuatayo–
- kukiuka kwa hali ya juu Vifungu vya Katiba au sheria nyingine yoyote;
- kwa kuwa kuna sababu kali za kuamini kwamba Waziri amefanya kosa la jinai chini ya sheria za kitaifa na kimataifa; au
- kwa kuwa na utovu wa nidhamu wa hali ya juu.
Utaratibu wa kumwondoa Waziri afisini
Iwapo mjadala wa kumwondoa Waziri afisini utaungwa mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge wote wa Baraza la Kitaifa–
- Bunge litateua kamati maalumu itakayokuwa na wanachama kumi na mmoja kuchunguza suala hili; na
- katika muda wa siku kumi, kamati hii maalumu itaripoti kwa Baraza la Kitaifa ikiwa limepata iwapo madai dhidi ya Waziri ni ya kuthibitika.
Waziri ana haki ya kwenda au kuwakilishwa mbele ya kamati maalumu wakati wa uchunguzi wake.
Iwapo kamati maalumu itaripoti kwamba imepata madai–
- hayathibitiki, hakuna taratibu nyingine zitakazochukuliwa; ama
- yamethibitika, Baraza la Kitaifa–
- litampa Waziri nafasi ya kusikizwa; na
- litapiga kura kama litaidhinisha uamuzi unaomtaka Waziri kuachishwa kazi.
Iwapo uamuzi unaomtaka Rais kumwachiza kazi Waziri, utaungwa mkono na wingi wa wabunge wa Baraza la Kitaifa–
- Spika (wa Baraza la Kitaifa) kwa haraka atawasilisha uamuzi huu kwa Rais; na
- Rais atamwachisha kazi Waziri.
Waziri atasalia afisini iwapo madai dhidi yake hayadhibitiki.