Kifungu cha 88 cha Katiba ya Kenya kinaanzisha na kubainisha jukumu la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.
Jukumu la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ni kuendesha au kusimamia kura za maoni na uchaguzi wa chombo chochote cha kuchaguliwa au ofisi iliyoanzishwa na Katiba, na uchaguzi mwingine wozote kama ilivyoainishwa na Sheria ya Bunge.
Jedwali la Yaliyomo Onyesha/Ficha
Muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka
Uanachama wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka unapaswa kuwa na mwenyekiti na wanachama wengine sita walioteuliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 250 (4) cha Katiba na masharti ya Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.
Mtu yeyote anaweza kuteuliwa kuwa mwanachama wa Tume ya Uchaguzi ikiwa mtu huyo-
- ana shahada kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa;
- amethibitisha uzoefu unaofaa katika mojawapo ya nyanja zifuatazo-
- mambo ya uchaguzi;
- usimamizi;
- fedha;
- utawala;
- utawala wa umma;
- sheria; na
- anakidhi matakwa ya Sura ya Sita ya Katiba.
Mtu hastahili kuteuliwa kuwa mwanachama wa Tume ya Uchaguzi ikiwa mtu huyo-
- amewahi, wakati wowote ndani ya miaka mitano iliyopita, kushika wadhifa, au kujitokeza kugombea kama–
- mbunge au mjumbe wa Baraza la Kaunti; au
- mwanachama wa baraza tawala la chama cha siasa; au
- anashikilia afisi yoyote ya serikali.
Mwanachama wa Tume ya Uchaguzi hapaswi kushika wadhifa mwingine wa umma.
Wanachama wa Tume wanapaswa kuteuliwa kwa muhula mmoja wa miaka sita na hawastahili kuteuliwa tena. Wanapaswa kuhudumu kwa muda wote.
Mwenyekiti na wanachama wa Tume ya Uchaguzi wanafaa kutekeleza majukumu yao kama ilivyoainishwa katika Katiba, na sekretarieti ya Tume ifanye kazi za kiutawala za kila siku za Tume.
Utaratibu wa kubadilisha nafasi ya mwenyekiti au mwanachama wa Tume unafaa uanze angalau miezi sita kabla ya mwisho wa muda wa mwenyekiti au mwanachama wa Tume.
Afisi ya mwenyekiti au mwanachama wa Tume itakuwa wazi iwapo yeye-
- hufa;
- anajiuzulu afisi kwa notisi iliyoandikwa kwa Rais; au
- anaondolewa afisini chini ya hali yoyote iliyotajwa katika Kifungu cha 251 na Sura ya Sita ya Katiba.
Kazi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka
Kifungu cha 88 (4) cha Katiba ya Kenya kinabainisha wajibu na kazi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya.
Tume ina jukumu la kuendesha au kusimamia kura za maoni na uchaguzi wa chombo chochote cha uchaguzi au afisi yoyote iliyoanzishwa na Katiba, na uchaguzi mwingine wowote kama ilivyoainishwa na Sheria ya Bunge na, hususan, kwa–
- usajili endelevu wa raia kama wapiga kura;
- marekebisho ya mara kwa mara ya orodha ya wapiga kura;
- uwekaji mipaka ya maeneo bunge na wadi kwa mujibu wa Katiba;
- udhibiti wa utaratibu ambao vyama vinateua wagombeaji kwa ajili ya uchaguzi;
- utatuzi wa mizozo ya uchaguzi, ikijumuisha mizozo inayohusiana na au inayotokana na uteuzi, lakini bila kujumuisha malalamiko na migogoro ya uchaguzi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi;
- usajili wa wagombea wa uchaguzi;
- elimu ya wapiga kura;
- kuwezesha uangalizi, ufuatiliaji na tathmini ya uchaguzi;
- udhibiti wa kiasi cha pesa ambacho kinaweza kutumiwa na au kwa niaba ya mgombea au chama kuhusiana na uchaguzi wowote;
- uundaji na utekelezaji wa kanuni za maadili kwa wagombea na vyama vinavyoshiriki uchaguzi;
- ufuatiliaji wa utiifu wa sheria inayotakiwa na Ibara ya 82(1) (b) ya Katiba inayohusiana na uteuzi wa wagombea na vyama;
- matumizi ya teknolojia na mbinu zinazofaa katika utendaji wa kazi zake; na
- majukumu mengine kama yalivyoainishwa na Katiba au sheria nyingine yoyote iliyoandikwa.
Kwa habari zaidi kuhusu jukumu la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, na Tume kwa ujumla, tazama Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka(Kiungo cha Nje) au tembelea tovuti yao.