Sura ya 5 ya Katiba inahusu uainishaji wa ardhi nchini Kenya. Kifungu cha 60 cha Katiba ya Kenya kinahusu kanuni za sera ya ardhi.
Ardhi nchini Kenya inafaa kushikiliwa, kutumiwa na kusimamiwa katika misingi ya usawa, ufanisi, uzalishaji na uendelevu, na kwa mujibu kanuni zifuatazo–
- uwezo sawa wa kupata ardhi;
- usalama wa haki za ardhi;
- usimamizi endelevu na wa manufaa, wa rasilmali za ardhi;
- usimamizi wa ardhi kwa uwazi na kwa gharama ya kufaa;
- hifadhi na utunzaji bora wa maeneo muhimu kiekolojia;
- kumaliza ubaguzi wa kijinsia katika sheria, mila na desturi zinazohusiana na mali iliyomo katika ardhi hiyo; na
- kuhimiza jamii kutatua mizozo kuhusu ardhi kupitia mifumo ya kiasili inayoambatana na Katiba.
Kanuni hizi ziafaa kutekelezwa kupitia kwa sera ya ardhi ya kitaifa inayoundwa na kuchunguzwa upya kila mara na serikali ya kitaifa kupitia kwa sheria.
Jedwali la Yaliyomo Onyesha/Ficha
Uainishaji wa Ardhi nchini Kenya
Kifungu cha 61 cha Katiba kinasema kwamba ardhi yote nchini Kenya ni ya Wakenya wote kama taifa, jamii na kama watu binafsi.
Kwa hivyo, uainishaji wa ardhi nchini Kenya ni ardhi ya umma, ardhi ya jamii au ardhi ya kibinafsi.
Ardhi ya Umma
Kifungu cha 62 cha Katiba kinafafanua ardhi ya umma nchini Kenya. Ardhi ya umma ni–
- (a) ardhi ambayo wakati wa kuanza kutumika kwa Katiba ni mali ya Serikali inavyoelezwa na Sheria ya Bunge wakati huo;
- (b) ardhi inayomilikiwa, kutumiwa au kukaliwa kisheria na taasisi yoyote ya Serikali, isipokuwa pale ambapo ardhi hiyo inakaliwa na idara ya Serikali chini ya kukodi kibinafsi;
- (c) ardhi iliyokabidhiwa Serikali kwa njia ya kuuza, kurudishiwa au kusalimishwa;
- (d) ardhi ambayo haimilikiwi kisheria na mtu yeyote au jamii yoyote;
- (e) ardhi ambayo mrithi wake hawezi kutambuliwa kwa vyovyote kisheria;
- (f) ardhi yoyote iliyo na madini au mafuta inavyoelezwa kisheria;
- (g) misitu ya Serikali kando na misitu inayotajwa katika Kifungu cha 63 (2) (d) (i) (angalia pointi ya 4 chini ya ardhi ya jamii), hifadhi ya wanyama, chemichemi za maji, mbuga za kitaifa, hifadhi za wanyama za serikali na sehemu maalum zilizolindwa;
- (h) barabara zote kulingana na Sheria ya Bunge;
- (i) mito yote, maziwa yote na sehemu nyingine za maji kama inavyoelezwa na Sheria ya Bunge;
- (j) mipaka ya bahari, maeneo maalum ya kiuchumi na chini ya bahari;
- (k) miamba ya kibara;
- (l) ardhi yote kati ya nyanda za juu na za chini za maji;
- (m) ardhi yoyote ambayo haijaainishwa kama ya kibinafsi au ya jamii chini ya Katiba; na
- (n) ardhi yoyote itakayotangazwa kuwa ya umma na Sheria ya Bunge–
- (i) itakayotumika katika tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba; na
- (ii) iliyoidhinishwa baada ya kuanza kutumika kwa Katiba.
Ibara ya 62(2) ya Katiba inaeleza kuwa ardhi ya umma itatolewa na kumilikiwa na Serikali ya Kaunti kwa amana kwa niaba ya wakazi wa Kaunti hiyo na itasimamiwa kwa niaba yao na Tume ya Kitaifa ya Ardhi iwapo imeainishwa chini ya–
(a) ibara ya (a), (c), (d) au (e) hapo juu; na (b) ibara ya (b) mbali na ardhi inayoshikiliwa, inayotumiwa au inayomilikiwa na idara za Serikali ya kitaifa.
Ardhi ya umma, inayoainishwa chini ya ibara ya (f) hadi (m) itatolewa na kumilikiwa na Serikali ya kitaifa kwa amana kwa niaba ya wananchi wa Kenya na itasimamiwa kwa niaba yao na Tume ya Kitaifa ya Ardhi.
Ardhi ya umma haitatolewa au kutumiwa isipokuwa kwa kuzingatia Sheria ya Bunge (Sheria ya Ardhi) inayofafanua hali na masharti ya kutolewa au matumizi hayo.
Ardhi ya Jamii
Kiungu cha 263 cha Katiba kinasisitiza kuwa ardhi ya jamii itatolewa na kumilikiwa na jamii zinazotambuliwa kwa misingi ya kikabila, kitamaduni au mahitaji ya kijamii yanayofanana.
(2) Ardhi ya jamii inahusisha–
- ardhi iliyosajiliwa kwa jina la wawakilishi wa kikundi kilicho chini ya masharti ya sheria yoyote;
- ardhi yoyote iliyokabidhiwa jamii fulani kupitia kwa njia yoyote ya kisheria;
- ardhi nyingine yoyote itakayotangazwa na Sheria ya Bunge kama ardhi ya jamii; na
- ardhi –
- (i) inamilikiwa kihalali , kusimamiwa au kutumiwa na jamii maalum kama misitu ya jamii, malisho ya mifugo au madhabahu;
- (ii) ardhi ya kinasaba na ardhi ambayo kitamaduni ilimilikiwa na jamii ya wawindaji; au
- (iii) kisheria inashikiliwa kama ardhi ya amana na serikali za Kaunti lakini isiyojumuisha ardhi ya umma iliyoshikiliwa kama amana na serikali za kaunti chini ya Kifungu cha 62 (2) cha Katiba.
Ardhi yoyote ya jamii ambayo haijasajiliwa itashikiliwa kwa amana na Serikali za kaunti kwa niaba ya jamii hizo.
Ardhi ya jamii haitatolewa au kutumiwa vinginevyo isipokuwa kwa misingi ya sheria inayofafanua hali na viwango vya haki za kila mwanajamii kibinafsi au wanajamii wote kwa pamoja.
Bunge litatunga sheria kuidhinisha utekelezwaji wa Kifungu cha 63 (kwa hiyo Sheria ya Ardhi ya Jamii(Kiungo cha Nje)).
Ardhi ya kibinafsi
Ardhi ya kibinafsi inajumuisha–
- ardhi yoyote iliyosajiliwa na inayomilikiwa na mtu yeyote chini ya umilikaji ardhi bila masharti;
- ardhi inayomilikiwa na mtu yeyote kwa kukodisha; na
- ardhi yoyote nyingine iliyotangazwa kuwa ya kibinafsi chini ya Sheria ya Bunge.
Ili kujifunza zaidi kuhusu uainishaji wa ardhi nchini Kenya na ardhi kwa ujumla, tazama Sheria ya Ardhi(Kiungo cha Nje) na sura ya Tano ya Katiba.